Rais wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak, na watoto wake wawili wa kiume, wamekana kuhusika na ufisadi hivi leo, wakati walipopandishwa tena kizimbani kujibu upya tuhuma dhidi yao. Jaji wa Mahakama ya Uhalifu mjini Cairo aliwauliza wote watatu, ikiwa walifanya ubadhirifu wa fedha za serikali, lakini wakajibu kwa pamoja kwamba jambo hilo halikuwahi kutokea. Mubarak na wanawe Alaa na Gamal, kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka ya kutumia dola milioni 14 za serikali, kwa ajili ya nyumba zao binafsi. Gazeti la al-Masry al-Youm, limeandika kwamba mwendesha mashitaka, aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa hao. Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi tarehe 29 mwezi huu. Awali, Mubarak, aliyeitawala Misri kwa takribani miaka 30, hadi alipopinduliwa na umma mwaka 2011, alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu kwa mashitaka hayo, huku wanawe wakihukumiwa miaka minne kila mmoja, lakini mahakama ya juu ya rufaa ikaamuru kurejewa upya kwa kesi hiyo, mwezi Januari mwaka huu.
4 Aprili 2015 - 19:47
Msimbo wa Habari: 681238
Rais wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak, na watoto wake wawili wa kiume, wamekana kuhusika na ufisadi hivi leo, wakati walipopandishwa tena kizimbani kujibu upya tuhuma dhidi yao.