Serikali ya Uturuki imemuita nyumbani balozi wake wa makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani Vatican, baada ya kiongozi wa kanisa hilo Papa Francis kuyataja mauaji ya waarmenia katika vita vya kwanza vikuu vya dunia kuwa ya halaiki.Vyombo vya habari nchini Uturuki vimeripoti balozi huyo ametakiwa kurejea nyumbani kuonyesha kughadhabishwa kwa Uturuki na matamshi ya Papa. Kiongozi huyo wa kanisa Katoliki amesema katika Kumbukumbu ya 100 ya mauaji ya watu wa jamii ya warmenia kuwa mauaji hayo yaliyofanyika mwaka 1915 ni ya kwanza ya halaiki katika karne ya ishirini. Uturuki imesema imesikitishwa mno na kuvunjwa moyo na matamshi hayo ambayo imesema imesababisha kuwepo kwa tatizo la uaminifu kati yake na Vatican.