Kumetokea upinzani mkali dhidi ya rais Nkurunziza ambaye anataka kugombea urais wa nchi hiyo kwa awamu ya tatu.
Watu wawili wameuawa baada ya kupigwa risasi na polisi nchini Burundi.
Watu hao walikuwa wanaandamana kupinga uamuzi wa chama kinachotawala nchini humo CNDD-FDD wa kumteua Rais Pierre Nkurunziza kuwa mjumbe wake katika uchaguzi wa rais utakaofanyika tarehe 26 mwezi Juni.Rais Nkurunziza ameshaitumikia mihula miwili ya urais,na wapinzani na mashirika ya haki za binadamu yanasema mpango wake wa kuwania muhula wa tatu unaenda kinyume na katiba.
Watu hao wawili walipigwa risasi na polisi wakati polisi hao walipokuwa wanajaribu kuwatawanya watu waliokuwa wanafanya maandamano yaliyopigwa marufuku .