Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Wapiganaji wa Kikurdi wakisaidiwa na vikundi vya waasi ambavyo Marekani inaviita kuwa ni magaidi wasio na hatari, wakiongozwa na wanajeshi wa Marekani wamekabiliana na kundi la kigaidi la Daesh katika ngome yao mjini Raqa nchini Syria.
Wakati hayo yanajiri vikosi vya Iraq vikiongozwa na wataalamu wa vita kutoka Iran vinafanya mashambulizi kuukomboa mji wa Fallujah, Iraq.
Operesheni hizo mbili dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh zimeelezwa kuwa muhimu katika kuwavunja nguvu wanamgambo wa kundi hilo tangu lilipotangaza utawala wa kiislamu nchini Iraq na Syria mwaka 2014.
Asilimia kubwa ya wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh kabla ya kuasi walipata mafunzo kutoka jeshi la Marekani kwa lengo la kuiangusha serikali ya Libya na hatimaye wakatumwa Syria kwa lengo la kuangusha serikali ya Bashar asad, kwa sasa Marekani na washirika wake wameanzisha muungano wa kijeshi kwa madai ya kupambana na kundi hilo.
Muungano huo unapita katika vijiji na maeneo ya mashamba kusini mwa mji wa Ain Issa, kilometa 60 hivi kutoka Raqqa na umevikomboa vijiji vitano na mashamba manne.
Shirika linalofuatilia masuala ya haki za binadamu nchini Syria limesema leo kwamba muungano unaoongozwa na Marekani umefanya mashambulizi yasiyopungua 150 dhidi ya wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh katika miji ya Tal Abyad na Ain Issa tangu operesheni ilipoanza Jumanne wiki hii. Shirika hilo pia limesema wapiganaji wapatao 31 wa kundi la kigaidi la Daesh wameuliwa katika makabiliano kaskazini mwa mkoa wa Raqa.
Muungano unaoongozwa na Marekani umekuwa ni muungano dhaifu licha ya kukusanya nchi Zaidi ya 60, tofauti na muungano wa Urusi ambao umekusanya nchi tatu tu lakini wameweza kulivunja nguvu kundi hilo la kigaidi katika kipindi kifupi sana.
Hakuna terehe ya kufanyika mazungumzo ya amani
Huku haya yakiarifiwa, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mzozo wa Syria Staffan de Mistura alisema mazungumzo kuhusu mzozo huo hayatafanyika katika wiki zijazo. De Mistura amelifahamisha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu azma yake ya kuanza duru nyingine ya mazungumzo haraka iwezekanavyo, lakini si katika wiki mbili au tatu zijazo.
Mjumbe huyo alielezea kuvunjwa moyo na ugumu uliopo katika kutoa huduma za kibinadamu Syria, hatari kubwa inayoukabili mkataba wa kusitisha uhasama, na haja ya kuhakikisha mazungumzo ya kisiasa yanapiga hatua.
De Mistura ataendelea kuwasiliana na pande zinazohasimiana pamoja na kushauriana na kundi la kimataifa linalosaidia juhudi za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Syria, mpaka atakapokuwa katika nafasi ya kuamua juu ya wakati muafaka wa kuanza mazungumzo.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Samantha Power, alisema Marekani ina wasiwasi kuhusu hali ya kukata tamaa nchini Syria. Power alidokeza kwamba machafuko yameongezeka katika mwezi uliopita na ni dhahiri kitisho kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kinasababishwa na utawala wa Syria na washirika wake, na kile alichokiita kuwa mashambulizi dhidi ya raia.
"Urusi ina jukumu maalumu kuushinikiza utawala wa Syria kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano na kukomesha mashambulizi ya mabomu na kuwazingira raia wa Syria wasio na hatia," aliongeza Power.
Marekani na washirika wake wamekuwa wakiyapatia silaha makundi ya kigaidi nchini Syria ili yaiangushe serikali halali ya Syria kama walivyofanya nchini Libya, lakini Urusi na Iran zimeahidi kuilinda serikali ya Syria na wananchi wake na kutoruhusu Marekani na washirika wake kufanya uharibifu kama Libya.
Kaburi la pamoja lagunduliwa
Wakati huo huo, shirika la haki za binadamu la Syria limesema kaburi la pamoja lenye maiti kiasi 65 za watu waliouliwa na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Daesh limegunduliwa na vikosi vya serikali karibu na uwanja wa ndege wa jeshi katika mji mkongwe wa Palmyra.
Shirika hilo limesema maiti hizo ni za wanachama wa vikosi vya serikali na nchi washirika walioonyongwa baada ya kundi la kigaidi la Daesh kuuteka na kuudhibiti mji wa Palmyra Mei 2015. Serikali ya Syria mjini Damascus haijathibitisha taarifa hizo.
Kundi la kigaidi la Daesh lilikamata mji huo kipindi ambacho ndege za Marekani zikiranda juu ya anga ambalo magaidi hao wanaua wananchi kinyama, bila ya ndege hizo kuwashambulia magaidi hao, jambo lilipelekea serikali ya Iran kuongoza wataalamu wake wa vita nchini Syria na Iraq ili kupambana na magaidi hao wanaoungwa mkono na Marekani.
Mwisho wa habari/ 291