9 Juni 2019 - 07:43
WHO: Wengi DRC hawajui wanaugua Ebola

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema karibu robo ya walioambukizwa Ebola huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamkini hawajui wanaugua ugonjwa huo hatari.

(ABNA24.com) Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema karibu robo ya walioambukizwa Ebola huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamkini hawajui wanaugua ugonjwa huo hatari.

Katika taarifa WHO imesema kuwa mtu mmoja kati ya wanne mashariki mwa DRC, ameambukizwa ugonjwa hatari wa Ebola lakini hafahamu.

WHO imesema hilo wakati huu inapoendelea kusaidia kupambana na maambukizi ya Ebola hasa mjini Beni, ambapo watu zaidi ya 2,000 wameambukizwa na wengine 1,357 wamepoteza maisha tangu mwezi Agosti mwaka 2018.

Hivi karibuni pia Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC ilitahadahrisha kuhusu tishio la ugonjwa hatari wa Ebola kuenea katika nchi za jumuiya hiyo.

EAC imesema Ebola bado ni tishio kubwa kwa watu wa Afrika Mashariki, na kuonya kuhusu matokeo mabaya ya ugonjwa huo kwenye kilimo, utalii na maisha ya watu wa kanda hiyo.

Mfumuko mkubwa zaidi wa ugonjwa wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za magharibi mwa Afrika za Guinea, Liberia na Sierra Leone.





/129