15 Juni 2019 - 07:36
Rais Tayyip Erdoğan: Mwezi ujao Uturuki itapokea ngao ya makombora ya S-400 ya Russia

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa, mwezi ujao wa Julai Russia itaikabidhi nchi yake ngao ya kiulinzi ya makombora ya S-400.

(ABNA24.com) Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa, mwezi ujao wa Julai Russia itaikabidhi nchi yake ngao ya kiulinzi ya makombora ya S-400.

Erdoğan ameihutubu Marekani akisema kwamba, Uturuki lazima itanunua ngao hiyo ya makombora kutoka Russia. Kabla ya hapo pia kiongozi huyo wa Uturuki alitoa sisitizo kama hilo kwamba Ankara itanunua ngao hiyo ya makombora licha ya mashinikizo mbalimbali ya Marekani.

Hayo yanajiri ambapo katika miezi ya hivi karibuni Marekani na Uturuki zimeingia katika hitilafu kubwa kuhusiana na masuala tofauti, ikiwemo kadhia ya ununuzi wa ngao ya makombora ya S-400 iliyotengenezwa nchini Russia.

Katika uwanja huo Patrick M. Shanahan, Kaimu Waziri wa Ulinzi wa Marekani Jumatano ya jana alitangaza kwamba, iwapo serikali ya Uturuki haitabadili msimamo wake kuhusiana na suala la ununuzi wa ngao hiyo ya makombora kutoka Russia, Washington itasimamisha ushirikiano wake na Ankara katika uzalishaji wa ndege za kivita za F-35.

Marekani inadai kwamba, usimikaji wa ngao ya makombora ya S-400 ndani ya ardhi ya Uturuki utafichua nukta za udhaifu wa ndege za Marekani za F-35 kwa hasimu wake Russia. Mkataba wa mauziano ya ngao hiyo ya makombora kati ya Ankara na Moscow ulitiwa saini Disemba 2017. Ngao ya anga na ardhini ya S-400 ina uwezo wa kufyatua makombora 72 kwa wakati mmoja na kulenga shabaha umbali wa kilometa 60 na kwa muinuko wa kilometa 27. Kwa ajili hiyo inatajwa kuwa miongoni mwa ngao za kisasa zaidi za makombora duniani.



/129