(ABNA24.com) Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa, wahusika wa mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mkosoaji wa utawala wa Aal-Saud, watalipa gharama nzito.
Rais Erdoğan ameyasema hayo leo katika radiamali yake kufuatia ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyomuhusisha Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia na mauaji ya Jamal Khashoggi ambapo amebainisha kwamba ripoti hiyo inawahusisha moja kwa moja watawala wa Saudi Arabia na mauaji ya mwandishi huyo na kwamba mtazamo wa Saudia kuihusu Uturuki, ni mtazamo wa kimakosa. Wakati huo huo, Lindsey Graham, Seneta wa chama cha Republican wa jimbo la Carolina Kusini nchini Marekani, sambamba na kukinaika na ripoti ya Umoja wa Mataifa juu ya kuhusika Mohammad Bin Salman na mauaji ya Jamal Khashoggi, amesisitiza kuwa yule aliyemuua mwandishi huyo wa habari ni Mrithi huyo wa Kiti cha Ufalme wa Saudia.
Agnes Callamard Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano alitangaza kwamba ushahidi wa kuaminika unaonyesha kuhusika viongozi wa ngazi za juu wa Saudia akiwemo Mohammad Bin Salman katika jinai ya mauaji ya Khashoggi. Itakumbukwa kuwa Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mkosoaji wa utawala wa Saudia, aliuawa tarehe pili Oktoba mwaka jana ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki kwa namna ya kutisha sana. Mwandishi huyo aliuawa na maafisa usalama wa Saudia, waliotumwa rasmi kwa ajili ya kazi hiyo kutoka Riyadh.
/129
22 Juni 2019 - 05:55
Msimbo wa Habari: 953451
Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema kuwa, wahusika wa mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mkosoaji wa utawala wa Aal-Saud, watalipa gharama nzito.