9 Oktoba 2019 - 07:48
Jarida la Newsweek: Trump ameogopa vitisho vya Rais Erdoğan wa Uturuki kuhusu Syria

Jarida la Newsweek la Marekani limemnukuu mmoja wa viongozi wa serikali ya nchi hiyo akisema kuwa, Rais Donald Trump amesalimu amri mbele ya matakwa ya Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki kuhusiana na Syria na kuyakubali bila ya pingamizi lolote.

(ABNA24.com) Jarida hilo la kila wiki la nchini Marekani limeashiria mazungumzo ya hivi karibuni ya marais wa Marekani na Uturuki ambayo yalipelekea kutangazwa habari ya kurudi nyuma askari wa Kimarekani kutoka karibu na mpaka wa Uturuki na Syria na kumnukuu afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Washington akisema kuwa, Trump ameogopa vitisho vya Erdoğan na kukubali kiurahisi matakwa yake kuhusiana na Syria.

Afisa huyo wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe ameongeza kuwa, Trump ameshindwa katika mazungumzo yake na Erdoğan na kukubali kurejesha nyuma askari wa Marekani ili aonyeshe kuwa Washington imepata chochote, lakini ukweli ni kuwa Marekani haikuambulia chochote.

Afisa huyo wa serikali ya Marekani amelieleza jarida hilo kwamba, usalama wa taifa wa Marekani utakabiliwa na hatari inayoongezeka kila siku kwa miongo kadhaa lakini  rais wa nchi ni mtu dhaifu na asiye na ujasiri.

Baada ya mazungumzo ya simu siku ya Jumatatu iliyopita kati ya Rais Donald Trump na Rais Recep Tayyip Erdoğan, White House alitangaza kwamba, kwa kuzingatia uamuzi wa serikali ya Ankara kwa ajili ya kuanzisha operesheni za kijeshi katika maeneo yanayodhibitiwa na Wakurdi kaskazini mwa Syria, Washington imeamua kuwaondoa askari wake katika maeneo hayo.


/129