5 Novemba 2019 - 09:11
Rais Rouhani: Iran kuchukua hatua ya nne ya kupunguza uwajibikaji wake kwenye JCPOA

Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaanza kutekeleza hatua ya nne ya kupunguza uwajibikaji wake kwenya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kuanzia kesho.

(ABNA24.com) Rais Rouhani amesema hayo katika hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Ubunifu cha Azadi magharibi mwa mji mkuu wa Iran, Tehran ambapo amesisitiza kuwa, "Tutaanza kutekeleza hatua mpya kuanzia kesho, ambapo tutaanza kuweka gesi kwenye mashinepewa zetu za kisasa katika kituo cha Fordow."

Rais wa Iran amebainisha kuwa, taasisi husika zitaendelea kufuatilia hatua hizo za Iran ambazo anasisitiza kuwa zinaweza kuangaliwa upya. Amesema, "Iwapo upande wa pili utatekeleza wajibu wake, na sisi pia tutarejea katika kufungamana na JCPOA kikamilifu."

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, Ali Akbar Salehi anasisitiza kuwa, "Mashinepewa hizi za kizazi kipya zinaweza kurutubisha urani mara 10 zaidi ya mashinepewa za kizazi cha kwanza."

Kituo hicho cha ubunifu cha Azadi kilichozinduliwa hii leo na Rais wa Iran kitajikita zaidi katika masuala ya usanifu majengo, uzalishaji za dawa za nano, utafiti kuhusu utoaji wa huduma za afya kwa njia za kielektroniki, utafiti katika masuala ya bima na fedha, uwezekaji na utalii pamoja na masuala ya bioteknolojia.

Baada ya nchi za Ulaya kutochukua hatua za maana za kukabiliana na kujiondoa Marekani katika JCPOA, Iran hadi sasa imechukua hatua 3 za kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano hayo.

........
340