Miili ya wahamiaji 15, baadhi yao ikiwa imeungua, ilipatikana Ijumaa iliyopita katika eneo la pwani ya mji wa Sabratha, yapata umbali wa kilomita 70 kutoka mji mkuu Tripoli; eneo ambalo linatajwa kuwa nukta muhimu inayotumiwa na maelfu ya watu kila mwaka kuelekea katika pwani ya Italia.
Ripoti zinasema kuwa, maiti 11 za wahamiaji zilizoungua zilipatikana ndani ya boti huku maiti nyingine nne zilizokiwa na majeraha zikikutwa nje ya boti hiyo. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini LIbya (UNSMIL) umesema kuwa, japokuwa bado haijafahamika jinsi tukio hilo lilivyotokea, lakini mauaji hayo yanaaminika kuwa matokeao ya mapambano ya silaha kati ya magenge yanayojihusisha na biashara ya kuvusha watu. UNSMIL imezitaka mamlaka husika za Libya kuhakikisha kunafanyika uchunguzi wa haraka, ulio huru na wa wazi ili kuwafikisha wahalifu mbele ya vyombo vya sheria.
Maafa haya ni ukumbusho kamili wa ukosefu wa ulinzi unaowakabili wahamiaji na wanaotafuta hifadhi huko Libya, na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na magenge ya biashara haramu ya binadamu na mitandao ya uhalifu, umesema ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL).
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya ndani, wahamiaji hao, ambao wengi wao ni kutoka katika nchi za Kiafrika za chini ya Jangwa la Sahara, waliuawa Alhamisi iliyopita kwa kupigwa risasi kufuatia mzozo kati ya wafanya magendo haramu ya binadamu.
342/