12 Desemba 2025 - 16:34
Nakuru - Kenya | Khatibu wa Sala ya Ijumaa Sheikh Abdul Ghani Khatibu Aeleza Siri ya Utukufu wa Bibi Fatima (sa) kupitia Hadithi Tukufu za Mtume(saww)

Sheikh Abdul Ghani aliweka wazi kuwa mapenzi ya Mtume (saww) kwa Bibi Fatima (sa) hayawezi kuchukuliwa kwa mtazamo wa kawaida wa mapenzi ya baba kwa binti yake. Badala yake, ni tamko la kiungu na kijamii linalobainisha nafasi yake adhimu katika Uislamu.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Nakuru - KenyaKatika Sala ya Ijumaa iliyoongozwa leo na Sheikh Abdul Ghani Khatibu huko Nakuru, waumini walipata fursa ya kusikia mawaidha yenye uzito mkubwa kuhusu sifa, daraja na fadhila za Bibi Fatima Zahra (sa), binti mtukufu wa Mtume Muhammad (saww).

Sheikh Abdul Ghani aliweka wazi kuwa mapenzi ya Mtume (saww) kwa Bibi Fatima (sa) hayawezi kuchukuliwa kwa mtazamo wa kawaida wa mapenzi ya baba kwa binti yake. Badala yake, ni tamko la kiungu na kijamii linalobainisha nafasi yake adhimu katika Uislamu.

Khatibu alieleza kuwa Mtume (saww) alionyesha hadharani heshima na mapenzi kwa binti yake ili Umma ujifunze kielelezo bora cha mwanamke mwema, mchamungu na aliyekuwa imara katika kubeba jukumu la risala ya Mtume (s.a.w.w). Alisisitiza kuwa Bibi Fatima (sa) ndiye mwanamke bora kuliko wanawake wote wa ulimwenguni, kama alivyoelezwa na Mtume (saww) mwenyewe.

Fatima (s.a): Kielelezo na Tochi ya Umma

Katika khutba hiyo, Sheikh Abdul Ghani alibainisha kuwa Bibi Fatima (sa) ni tochi ya mwanga kwa Umma, anayemuongoza Mwislamu katika hatua zote za maisha. Alisema kuwa heshima yake kubwa ilitokana na jukumu alilobeba katika kuendeleza risala ya Uislamu baada ya kufariki kwa mama yake, Bibi Khadija (sa), hadi mwisho wa uhai wake.

Khatibu aliongeza kuwa Bibi Fatima (sa) alijitolea ipasavyo katika kufikisha, kutetea na kusimamia mafundisho ya Mtume (saww), bila kuchoka, jambo lililomfanya astahili kuitwa “Sayyidat Nisaa al-Alamina” – Mwanamke bora wa ulimwengu wote.

Kauli za Mtume (saww) Zilizoangaziwa

Miongoni mwa kauli za Mtume (saww) alizozinukuu ni pamoja na:

1_Fatima ni Sayyidat Nisaa al-Alamina

2_“Fatima ni mama wa baba yake.”

3_“Mwenyezi Mungu anaridhika kwa ridhaa za Fatima, na hukasirika kwa hasira zake.”

Kauli hizi, kwa mujibu wa Sheikh Abdul Ghani, zinaonesha sifa za juu zisizo na mfano alizonazo Bibi Fatima (sa) katika Uislamu.

Nakuru - Kenya | Khatibu wa Sala ya Ijumaa Sheikh Abdul Ghani Khatibu Aeleza Siri ya Utukufu wa Bibi Fatima (sa) kupitia Hadithi Tukufu za Mtume(saww)

Kwa kuhitimisha 

Khutba ilimalizika kwa wito kwa waumini kuishi kwa kufuata maadili, tabia na imani ya Bibi Fatima (sa) kama njia ya kujenga jamii yenye mwanga, utulivu na uchamungu.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha