30 Oktoba 2022 - 19:36
Wanajeshi 13 wameuawa katika shambulio la silaha mashariki mwa Burkina Faso

Wanajeshi 13 wameuawa katika shambulio la wanamgambo wenye silaha mashariki mwa Burkina Faso.

Burkina Faso katika miaka ya karibuni imekumbwa na mashambulizi mtawalia ya umwagaji damu; ambapo awali mashambulizi hayo yalianzia upande wa kaskazini mwa nchi na kisha kupanuka upande wa mashariki na katikati mwa nchi hiyo. Hadi sasa mamia ya raia wa kawaida na wanajeshi wameuawa katika hujuma za kigaidi nchini Burkina Faso.  

Hujuma hizo za kigaidi mara nyingi hushuhudiwa katika maeneo ya mipaka kati ya Burkina Faso na Mali, Niger na Benin. Duru za usalama za Burkina Faso leo zimetangza kuwa wanajeshi 13 wa nchi hiyo jana waliuawa wakati wanamgambo wenye misimamo mikali walipowavamia katika eneo moja mashariki mwa nchi hiyo. Wanajeshi wanne wa serikali ya Burkina Faso pia walijeruhiwa jana Jumamosi mashariki mwa nchi. Jumatatu iliyopita pia wanajeshi 28 waliuawa na 50 kujeruhiwa baada ya kambi yao kuvamiwa na watu wenye silaha kaskazini mwa nchi hiyo. 


342/