15 Novemba 2022 - 16:46
Baraza Kuu la Libya lakosoa hatua za Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo

Mkuu wa Baraza Kuu la Serikali ya Libya amesema kuwa, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya nchi hiyo anakwamisha mchakato wa kufanyika vikao vya baraza hilo.

Katika miezi ya karibuni Libya imeshuhudia mgogoro wa kisiasa ukipamba moto nchini humo huku Tripoli mji mkuu wa nchi hiyo ukigeuka na kuwa mahali pa kutumwa askari jeshi. Hali hiyo imeshuhudiwa ikiwa ni natija ya mapigano ya silaha yaliyosababishwa na hitilafu za kisiasa kati ya serikali mbili za nchi hiyo zinazoongozwa na Abdul Hamid al Dbeibah na serikali yenye mamlaka inayoongozwa na Fathi Bashaga.  

Khalid al Mishri Mkuu wa Baraza Kuu la Serikali ya Libya amemtuhumu Abdul Hamid al Dbeibah Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya nchi hiyo kuwa anakwamisha pakubwa utendaji wa Baraza Kuu la Libya. 

Al Mishri ametuma taarifa rasmi kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali na kuitaja serikali ya al Dbeibah ambayo muda wake wa kisheria wa uongozi umemalizika kuwa ni serikali ya wanamgambo na ya mafisadi. Amesema, serikali hiyo inafanya kila iwezalo kusalia madarakani. Tuhuma hizi zimetolewa wakati ambapo kundi lenye silaha la wafuasi wa Waziri Mkuu Abul Hamid al Dbeibah katika hatua ya nadra kushuhudiwa imeyazingira makao makuu ya Baraza Kuu la Uongozi la Libya na kuwazuia wajumbe wa baraza hilo kushiriki vikaoni. 

Khalid al Mishri amesisitiza kuwa, Baraza Kuu la Serikali ya Libya lilitazamia katika vikao vyake kuchunguza umoja wa Idara ya Utendaji na mchakato wa kisiasa wa Libya kwa ajili ya kufanyika uchaguzi sawa kabisa na kama ilivyopangwa kwa ajili ya kuwachagua wajumbe wapya kwa ajili ya nyadhifa muhimu za uongozi wa nchi ikiwemo pia nafasi ya juu zaidi ya Gavana wa Benki Kuu. 

342/