Main Title

source : Parstoday
Jumanne

27 Februari 2024

19:56:47
1440882

Afrika Kusini: UN iache undumakuwili katika kulaani ukiukwaji wa haki

Afrika Kusini imekosoa vikali undumakuwili wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa katika suala la kulaani ukanyagaji wa haki za binadamu duniani.

Akilihutubia baraza hilo jana Jumatatu, Naledi Pandor, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amezitaka nchi wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la UN kuachana na tabia ya kulaani kesi fulani za ukiukaji wa haki na wakati mwingine kupuuza kesi nyingine.

Amekosoa sera hizo za nyuso mbili za baadhi ya wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la UN na kueleza kuwa, "Wakati baadhi ya wanachama wanapozungumzia mgogoro wa Russia na Ukraine, wanauita uvamizi wa Russia, lakini inapokuja katika mashambulizi ya Israel dhidi ya Palestina, wanadai ni vita vya Israel dhidi ya HAMAS."

Pandor amesema utumiaji wa lugha hiyo unaipa Israel kibali cha kuwatazama Wapalestina wote kama wanachama wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, na kwa msingi huo wanastahili kuuawa.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Afrika Kusini amesisitiza kuwa, nchi zote wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa zina wajibu wa kuhakikisha kuwa taasisi hiyo inatekeleza majukumu yake kwa njia faafu.

342/