Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

7 Juni 2024

15:12:01
1463971

Kituo kikubwa zaidi cha anga za mbali Asia Magharibi kuanza kazi 2025 Iran

Ujenzi wa kituo kikubwa zaidi cha anga za mbali katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) unaendelea vizuri hapa nchini Iran, na kinatazimwa kuanza kazi zake mwaka ujao.

Hayo yamesemwa na Issa Zarepour, Waziri wa Teknlojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) katika ziara yake jana Alkhamisi katika kituo hicho kilichoko katika bandari wa Chabahar katika mkoa wa Sistan na Baluchistan, Kusini Mashariki mwa Iran na kuongeza kuwa, ujenzi wa kituo hicho umekamilika kwa asilimia 56. 

Waziri Zarepour amesema uzinduzi wa awamu ya kwanza ya kituo hicho cha anga za mbali cha Iran ambacho ndicho kikubwa zaidi Asia Magharibi utafanyika Februari mwaka ujao 2025.

Amesema kituo hicho mbali na kuiwezesha Iran kurusha satalaiti zake katika anga za mbali, lakini pia kitasaidia kuimarisha ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu na washirika wake wa kimataifa, sanjari na kuliongezea mapato taifa hili.

Iran hivi sasa inategemea Kituo cha Urushaji Satalaiti cha Imam Khomeini kilichoko katika mkoa wa kaskazini wa Semnan kurusha satalaiti na roketi la kubebea satalaiti katika anga za mbali. Kituo hicho kilizinduliwa rasmi mwaka 2017. 

Iran ni miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza duniani katika sekta ya anga za mbali, na mafanikio hayo ni matokeo ya zaidi ya miongo minne ya jitihada za wataalamu wa nchi hii ya Kiislamu, licha ya vikwazo na mashinikizo ya Marekani na waitifaki wake wa Magharibi.

Nchi za Magharibi zimekuwa zikionyesha kukasirishwa sana na hatua ya Iran kujitegemea kikamilifu katika uga wa satalaiti na anga za mbali.

342/