8 Juni 2024 - 18:23
Iran: Maafa ya Palestina hayataisha mpaka Marekani na Ulaya zitapoacha kuiunga mkono Israel

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Kusimamishwa kikamilifu na kivitendo uungaji mkono wa Marekani na Ulaya kwa utawala wa kibaguzi wa Kizayuni katika mashambulizi yake dhidi ya Ukanda wa Ghaza ndiko kunakoweza kukomesha maafa machungu na ukatili wa kinyama na unaofanywa bila kujali dhidi ya watu huko Palestina.

Nasser Kanani ameeleza hayo katika andiko aliloweka kwenye mtandao wa kijamii wa X alipogusia matamshi ya Joseph Borrell, Mkuu wa Sera za Nje za Umoja wa Ulaya kuhusu hali mbaya ya Ukanda wa Ghaza na akasema: "jinai za utawala wa kibaguzi dhidi ya raia wa Palestina, watoto na wanawake ziko wazi mbele ya macho ya watu wote duniani na bila ya shaka zinatisha na zinaungulisha nyoyo". Msemaji wa vyombo vya kidiplomasia vya Iran ameongeza kuwa: si kwa maneno tu, bali ni kwa kukomesha kikamilifu na kivitendo uungaji mkono wa Marekani na Ulaya kwa utawala wa kibaguzi wa Kizayuni, ndiko kutakokomesha maafa hayo machungu na ukatili wa kinyama na unaofanywa bila kujali dhidi ya watu huko Palestina.Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, amesema: "ripoti kutoka Ghaza zinaonyesha kuwa ukweli pekee unaotawala maisha ya mamia ya maelfu ya watu wasio na hatia ni ukatili na mateso. Kwa mujibu wa agizo la Mahakama ya Kimataifa ya Haki, kuna ulazima wa kufanywa uchunguzi huru kuhusu ripoti hizo".

 Wapalestina wasiopungua 36,654 wameuawa shahidi hadi sasa katika mashambulizi ya kinyama yaliyoanza kufanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza tangu tarehe 7 Oktoba 2023.../

342/