23 Septemba 2024 - 19:22
Rais wa Iran asema undumakuwili wa nchi za Magharibi ni sababu kuu za vita, mauaji

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amelaani misimamo ya undumakuwili ya nchi za Magharibi ambayo amesema imesababisha kuenea kwa umwagaji damu na vita duniani kote.

Rais wa Iran ameyasema hayo mapema Jumatatu alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa John F. Kennedy mjini New York, ambako anatarajiwa kuhutubia kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).

Kauli hiyo imekuja katika hali ambayo Marekani na nchi nyingine nyingi za Magharibi zinaunga mkono kisiasa na kijeshi Israel huku utawala huo ukiendelea na vita vya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza na hujuma za kila siku za mauaji dhidi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Lebanon na maeneo mengine ya kikanda.

Pezeshkian aidha amesema akiwa New York atawasilisha "ujumbe wa Iran kuhusu amani na usalama."

Kaulimbiu iliyopitishwa katika Mkutano Mkuu wa mwaka huu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ni, "Tusimwache Mtu Yeyote Nyuma: Kushirikiana kwa ajili ya Kuendeleza Amani, Maendeleo Endelevu, na Utu wa Binadamu kwa Vizazi vya Sasa na Vijavyo."

342/