Main Title

source : Pars Today
Jumapili

14 Julai 2019

08:56:30
960858

Ujasusi mpya wa serikali ya Marekani dhidi ya raia kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi

Baada ya mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani Serikali ya Federali ya nchi hiyo ilitunga sheria mpya za kudukua kumpyuta na mitandao ya intaneti ya raia ikisaidiwa na Kongresi kwa kisingizio...

(ABNA24.com) Baada ya mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani Serikali ya Federali ya nchi hiyo ilitunga sheria mpya za kudukua kumpyuta na mitandao ya intaneti ya raia ikisaidiwa na Kongresi kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Mwishoni mwa kipindi cha utawala wa Barack Obama zilifanyika jitihada za kupunguza udukuzi na operesheni hizo za ujasusi dhidi ya raia wa Marekani.

Hata hivyo katika kipindi cha utawala wa sasa wa Donald Trump suala la ujasusi wa serikali ya Marekani dhidi ya raia katika mtandao wa intaneti hususan mitandao ya kijamii, linaonekana kuchukua mkondo mpya. Katika uwanja huo Polisi ya Federali ya Marekani (FBI) inafanya mikakati ya kuzidisha udhibiti na usimamizi wa mitandao ya kijamii na kudukua taarifa kama za utambulisho wa watumiaji wa mitandao hiyo, adresi za IP na nambari zao za simu. Kwa sababu hiyo FBI tayari imesaini mkataba wa kutengeneza kifaa kipya cha usimamizi ambacho kitatumiwa kukusanya na kudukua taarifa zinazohitajiwa na polisi ya Marekani. FBI inadai kuwa, lengo la kutumiwa kifaa hicho ni kutambua na kudhibiti makundi ya kigaidi, kuchunguza vitisho vya ndani ya nchi, kufuatilia harakati za watenda jinai na kadhalika. Hata hivyo kuna hofu kwamba, kifaa hicho kitatumiwa kwa ajili ya kudukua na kuingilia masuala binafsi ya mabilioni ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kote duniani.

Suala hilo limetambuliwa kuwa nyeti mno kwa kutilia maanani kashfa iliyofichuliwa mwaka 2013 na mfanyakazi wa zamani wa Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani (NSA) Edward Snowden kuhusu ujasusi mkubwa unaofanywa na taasisi za usalama na ujasusi za Marekani hususan shirika hilo la NSA dhidi ya raia wa nchi hiyo na nchi nyingine duniani bali hata viongozi na marais wa nchi mbalimbali. Mwezi Juni mwaka 2013 Snowden alifichua miradi yenye usiri mkubwa ya aina mbili ya serikali ya Marekani. Katika fremu ya miradi hiyo Shirika la Usalama wa Taifa la Marekani (NSA) na Polisi ya Federali (FBI) zimekuwa zikidukua na kufuatilia mazungumzo ya simu ya mamilioni ya watu ndani ya nchi hiyo na barani Ulaya na kunasa na kujasisi taarifa za mitandao ya intaneti za mamia ya makampuni makubwa kama Facebook, Google, Apple na Microsoft. Snowden alifichua kwamba, shirika la NSA linafanya ujasusi kwa raia wa Marekani kuliko raia wa nchi za kigeni. Aliongeza kusema kuwa: "Sisi tunawafanyia ujasusi na kuwafuatilia raia wetu wenyewe kuliko watu wengine duniani."

Polisi ya Federali nayo inakusanya taarifa za mazungumzo ya simu na mawasiliano ya mitandao ya intaneti ya raia wa Marekani kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Kifaa kipya cha FBI ni chombo cha taasisi hiyo cha kupenya na kuingia katika adresi za watumiaji wa mitandao ya kijamii na kinawawezesha majasusi wa FBI kupata adresi za baruapepe, utambulisho halisi wa watumiaji wa intaneti, nambari zao za simu na kadhalika. Vilevile kinawawezesha makachero wa mashirika ya ujasusi ya Marekani kufuatilia maeneo na mahali mlengwa anapokuwa na kujua historia ya kila mtu ya kutumia mitandao ya kijamii.

Inatarajiwa kuwa hatua hiyo ya Polisi ya Federali ya Marekani itakabiliwa na upinzani mkubwa wa watumiaji wa mitandao ya kijamii na raia kwa ujumla ambao wana wasiwasi kwamba, mashirika hayo ya ujasusi yatatumia vibaya taarifa zinazohusiana na maisha yao binafsi na kuingilia mambo yao makhsusi.




/129