(ABNA24.com) Hatua hiyo iliamsha hasira ya wabunge wa Marekani ambao wamekuwa wakifanya juhudi za kusimamisha mauzi hayo ya silaha. Baada ya Seneti ya Marekani kupinga mauzo hayo makubwa ya silaha, bunge la Congress pia Jumatano iliyopita lilipitisha mswada wa kupiga marufuku mauzo hayo ya silaha kwa Saudia na Imarati. Seneti ilikuwa imepitisha mswada wa kupiga marufu mauzo hayo ya silaha mwezi Juni uliopita.
Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani mwezi Mei alikuwa amethibitisha kuwepo kwa mikata 22 ya mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia, Imarati na Jordan kwa kisingizio kwamba kulikuwepo na tangazo la hali ya hatari kwa usalama wa taifa. Serikali ya Trump ilijaribu kutumia kisingizio jicho kukwepa vizingiti vya Congress. Katika hali ya kawaida Cogress huwa ina muda wa siku 30 kuchunguza miamala ya aina hiyo ya mauzo ya silaha.
Eliot Engel, mbunge wa chama cha Democrat anayeliwakilisha jimbo la New York na ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya bunge inayoshughulikia masuala ya kigeni amesema kwamba iwapo serikali inataka kuuza silaha hizo inapasa kufuata sheria na sio kuitumia vibaya.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miezi miwili iliyopita kwa Congress kupasisha muswada dhidi ya uhusiano maalumu uliopo baina ya serikali ya Trump na utawala wa Saudia. Mwezi Aprili mwaka huu pia, wabunge wa Marekani walipitisha muswada wa kusimamisha ushirikiano wa serikali ya nchi hiyo na Saudia katika vita vya kichokozi vinavyoendeshwa na nchi hiyo dhidi ya jirani yake Yemen. Wabunge wa Seneti kutoka vyama vyote viwili vya Democrat na Republican walionyesha kuchukizwa kwao kutokana na uamuzi wa serikali ya Donald Trump wa kuitenga Congress katika kutangaza hali ya hatari nchini. Katika kutangazwa hali ya hatari kwa usalama wa taifa, rais wa Marekani anaruhusiwa kupuuza sheria zinazohusiana na udhibiti wa silaha na kuuza silaha bila kibali cha Congress.
Wabunge wa vyama vyote viwili vya Democrat na Republican wamekerwa na hatua ya Trump ya kuendelea kuwa na ushirikiano mkubwa na watawala wa Saudia na kusisitiza kuwauazia silaha kwa wingi, licha ya watala hao kuhusika moja kwa moja katika mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi mkosoaji mkuu wa utawala wa Saudia, katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki.
Tarehe 15 mwezi huu pia Congress ilipitisha kwa wingi wa kura muswada wa kuadhibiwa wahusika wa mauaji ya Khashoggi.
Kuhusiana na suala hilo, Gazeti la New York Times liliandika hivi karibuni kwamba hakuna suala lolote jingine ambalo limezua mvutano mkubwa kati ya Trump na Congress katika siasa za nje kama lilivyofanya suala la Saudia.
Kuna uwezekano mkubwa kwamba Trump atatumia kura ya turufu kupinga muswada huo wa Congress kwa sababu siasa zake zimesimama katika msingi wa kuwa na uhusiano mkubwa na utawala wa Riyadh. Saudia ndio mshirika mkubwa wa kiuchumi na kistratijia na pia mnunuzi mkubwa zaidi wa silaja za Marekani katika eneo zima la Asia Magharibi. Imarati pia ni mmoja wa washirika muhimu wa Marekani katika eneo na kila mwaka hununua silaha nyingi kutoka nchi hiyo ya Magharibi. Hivyo ni wazi kuwa Trump hana nia yoyote ya kupunguza ushirikiano na nchi mbili hizo za Kiarabu, na hasa Saudia ambayo amekuwa akiidhalilisha mara kwa mara hadharani kwa kuitaja kuwa ni ngome ya kukamuliwa ambayo inapasa kukamuliwa hadi mwisho.
Kuhusiana na umuhimu wa kiuchumi wa Saudia kwa serikali ya Trump, inatosha kutaja hapa nukta hii kwamba mara tu baada ya kuingia White House, Trump alifanya safari yake ya kwanza nje ya nchi huko Saudia ambapo alitiliana saini na nchi hiyo ya kifalme mikataba muhimu ya mauzo ya silaha ya thamani ya dola bilioni 110.
/129