12 Mei 2020 - 10:53
Spika wa Bunge la Libya: Khalifa Haftar hatokuwa mshirika wetu wa kisiasa hapo baadaye

Spika wa bunge la Libya amebainisha kwamba, serikali ya Tripoli haimtambui Jenerali Khalifa Haftar kuwa mshirika wake wa kisiasa wa baadaye.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA:Hamouda Sayala, Spika wa Bunge lenye makao yake mjini Tripoti kwenye makao ya serikali ya mwafaka wa kitaifa ametoa taarifa na kubainisha kwamba, hakutakuwa na wito wowote wa kufanya mazungumzo na Haftar kabla ya yeye kuhitimisha operesheni za kijeshi. Sayala ameongeza kwamba iwapo jamii ya kimataifa haitachukua hatua kali ya kukabiliana na jinai za mauaji ya raia wasio na hatia kupitia mashambulizi ya kila siku yanayofanywa na wapiganaji wa Haftar, hakutakuwepo na mazungumzo yoyote hata kwa kusimamiwa na Umoja wa Mataifa. Aidha Spika huyo wa bunge la serikali ya mwafaka wa kitaifa amelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuitisha kikao cha dharura na kwa mujibu wa kipengee cha saba cha hati ya umoja huo, ili kutekeleza majukumu yake ya kulinda na kuwatetea raia wa Libya. Aidha Sayala amezitaja nchi zinazomuunga mkono Jenerali Khalifa Haftar kuwa ni watenda jinai. Wakati huo huo  Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imewaonya wapiganaji wa Khalifa Haftar wenye makao yao mashariki mwa Libya dhidi ya kufanya mashambulizi ya aina yoyote dhidi ya maslahi na wanadiplomasia wake nchini humo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imesema kuwa iwapo wapiganaji wa jenerali huyo muasi (Haftar) watashambulia maslahi au wanadiplomasia na maeneo ya kibalozi ya Uturuki nchini Libya, basi watakuwa wamejihalalishia kushambuliwa na jeshi la Uturuki. Awali Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki iliongeza kwamba mashambulizi ya wapiganaji wa Khalifa Haftar dhidi ya uwanja wa ndege wa Mitiga na jumbe za kidiplomasia yanahesabiwa kuwa jinai ya kivita. Uturuki imetoa onyo hilo katika hali ambayo Ahmed Al-Mismari, msemaji wa wapiganaji wa Haftar amesema kuwa zana zao za kukabiliana na mashambulizi ya anga, zimefanikiwa kutungua ndege isiyo na rubani ya Uturuki katika mji mkuu wa Libya, Tripoli. Siku ya Ijumaa vyombo vya habari vyenye mahusiano na wapiganaji wa jenerali huyo muasi vilitangaza habari ya kutunguliwa ndege hiyo isiyo na rubani, magharibi mwa mji wa Tripoli. Tangu ulipoondolewa madarakani utawala wa Kanali Muammar Gaddafi, kiongozi wa zamani wa Libya mwaka 2011, nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika imekuwa ikiongozwa na serikali mbili zenye makao makuu yao mashariki na magharibi mwa Libya.


342/