8 Julai 2020 - 10:39
Sisitizo la Russia juu ya mchango wa Marekani katika magendo ya madawa ya kulevya nchini Afghanistan

Mwaka 2001 Marekani iliishambulia kijeshi Afghanistan kwa kisingizio cha mashambulio ya Septemba 11 na ikaikalia kwa mabavu nchi hiyo.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Pamoja na hayo, uwepo wa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan haujawa na faida yoyote ghairi ya kuenea ugaidi, ukosefu wa usalama na amani, kukithiri umasikini na kubwa zaidi kuongezeka pakubwa uzalishaji pamoja na magendo ya madawa ya kulevya. Zamir Kabulov, mjumbe maalumu wa Russia katika masuala ya Afghanistan ametangaza kuwa, Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) limekuwa na nafasi na machango mkubwa katika biashara na magendo ya madawa ya kulevya nchini Afghanistan. Akitoa majibu kwa ripoti ya gazeti la New York Times lililodai kuweko njama za pamoja za Russia na wanamgambo wa Taliban katika kuwauwa wanajeshi wa Marekani, Kabulov amesema kuwa, shirika la CIA ambalo linaituhumu Russia, lenyewe ndilo linalohusika na magendo ya madawa ya kulevya.

Katika kuthibitisha madai yake hayo, mjumbe huyo maalumu wa Russia katika masuala ya Afghanistan amesema, ndege za Marekani kutoka Kandhar na Begram zimekuwa zikiruka na kutua bila upekuzi wowote katika maeneo ya Ujerumani na Romania na hii ni aina ya biashara. Nalo Shirika la Habari la Russia TASS limemnukuu Kabulov na kuandika kuwa, idadi kadhaa ya maafisa wa Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) ambalo linaituhumu Russia kupanga njama za Taliban wamekuwa wakijihusisha na magendo ya madawa ya kulevya nchini Afghanistan.

Kadhia ya kuenea kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa ulimaji wa mipopi na uzalishaji wa mihadarati nchini Afghanistan katika kipindi cha nchi hiyo kukaliwa kwa mabavu na uwepo wa majeshi ya Magharibi hususa ya Marekani pamoja na maafisawa kijasusi wa Marekani na Uingereza ni jambo ambalo limekuwa likizungumzwa na kujadiliwa kwa muda sasa. Viongozi wa Russia wamekosoa mara chungu nzima kigugumizi na kujizuia vikosi vya NATO na suala la kupambana na magendo ya mihadarati nchini Afghanistan.

Sergei Lavrov, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia Apirili mwaka 2017 alitangaza kuwa, Marekani na NATO zina mkono katika biashara ya mihadarati na magendo ya heroini kutoka Afghanistan na kuelekea katika mataifa mengine. Lavrov alisema bayana kwamba, Marekani na NATO zimekuwa zikiwatumia wanajeshi wake kwa ajili ya kulinda ulimaji wa mipopi, uzalishaji na magendo ya heroini na kuchukuliwa madawa hayo ya kulevya kutoka Afghanistan na kusambazwa katika mataifa mengine.

Lavrov ameashiria nukta hii kwamba, filihali asilimia 90 ya madawa ya kulevya aina ya heroini ulimwenguni yanatoka nchini Afghanistan  na kuituhumu Marekani kwamba, imepuuza kabisa jambo hilo na kueleza kuwa, takwimu hizi zinaonyesha juu ya kuweko uhuru kamili wa magendo ya madawa ya heroini nchini Afghanistan.

Serikali ya Moscow imetangaza mara kadhaa kwamba, mwenendo wa uzalishaji wa madawa ya kulevya nchini Afghanistan haujapungua hata kidogo. Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na uhalifu na mihadarati imetangaza katika ripoti yake ya kila mwaka kuwa, uzalishaji wa madawa ya kulevya nchini Afghanistan umeongezeka mno ambapo mwaka uliopita wa 2019 tani 6,700 za madawa ya kulevya yanayotokana na mpopi zilizalishwa nchini humo.

Kwa sasa Afghanistan ni miongoni mwa nchi za orodha ya kwanza katika ulimaji na uzalishji wa mihadarati ulimwenguni na mzalishaji mkubwa wa kasumba na mfano wa hivyo. Katika kipindi cha miaka 19 iliyopita, Marekani na Uingereza kwa kuweko kwao nchini Afghanistan zimekuwa na nafasi kubwa na ya wazi katika kukithiri na kuongezeka uzalishaji wa mihadarati katika nchi hiyo.

Viongozi wa Afganistan wanaamini kuwa, ukosefu wa usalama na kuzorota uchumi wa nchi hiyo chimbuko lake ni kuendelea ulimaji na uzalishaji wa madawa ya kulevya nchini humo na wametangaza kuwa, sekta hiyo inatishia usalama wa nchi kwani imekuwa chini ya udhibiti wa makundi pinzani yanayobeba silaha. Katika miaka ya nyuma, serikali ya Kabul  licha ya kupata msaada wa kimataifa na vikosi vya kigeni lakini haijafanikiwa kuzuia uzalishaji wa mipopi pamoja na magendo ya madawa ya kulevya nchini humo. Kwa mwaka magenge ya kimafia, wanamgambo wa Taliban na kundi la kigaidi la Daesh hupata faida ya  mabilioni ya dola kutokana na kufanya magendo ya mihadarati.

Licha ya madai na hatua za kujionyesha za Marekani katika uwanja wa kukabiliana na ulimaji mipopi na uzalishaji wa madawa ya kulevya nchini Afghanistan, kivitendo Wamarekani wenyewe ndio kizingizti kikuu katika vita dhidi ya mihadarati. Waheed Muzdha, mtaalamu wa masuala ya kisiasa na kijeshi wa Afghanistan anasema: Marekani ndilo chimbuko kuu la vita, uzalishaji wa mihadarati pamoja na magendo ya madawa hayo ya kulevya nchini Afghanistan.

Kwa utaratibu huo inaeleweka wazi kwamba, bila ya msaada wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja wa Wamarekani na kutopuuzwa ulimaji mkubwa wa mipopi katika maeneo mbalimbali nchini Afghanistan hasa katika maeneo kama Helmand vilipo vikosi vya Uingereza kivitendo haiwezekani kuibadilisha Afghanistan na kuifanya kuwa nchi kubwa zaidi duniani kwa uzalishai wa mipopi na kasumba. Hii ni katika hali ambayo, mataifa jirani au yaliyo karibu na Afghanistan kama Russia yanalazimika kuandaa wanajeshi na bajeti kubwa kila mwaka kwa ajili ya kuitumia katika vita dhidi ya magendo ya madawa ya kulevya yanayotoka nchini Afghanistan na kuingia katika nchi hizo.

Ukweli wa mambo ni kuwa, madawa ya kulevya yanayotoka nchini Afghanistan na kuingia nchini Russia kupitia nchi za Asia ya Kati, limekuwa tatizo kubwa kwa Moscow. Kwa muktadha huo, Marekani kwa kutoa baraka na ridhaa ya kuendelea kuzalishwa madawa ya kulevya nchini Afghanistan na vilevile kushiriki vikosi na maaafisa wake wa kiintelijensia katika magendo ya madawa ya kulevya yanayotoka Afghanistan, kivitendo imekuwa ikichukua hatua katika uwanja wa kuhatarisha usalama wa taifa wa mataifa hayo hususan Russia.

342/