9 Julai 2020 - 11:51
IMN: Kuna kiwango kikubwa cha sumu ya risasi katika damu ya Sheikh Zakzaky

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) imetangaza kuwa tathmini ya karibuni ya hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky inaonyesha kuwa kiwango cha mada ya risasi kilichoko katika mwili wa mwanazuoni huyo kiko juu kuliko kile kinachotarajiwa kwa binadamu.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wameeleza wasiwasi wao kuhusu hali ya kiafya inayoendelea kuwa mbaya ya kiongozi huyo na kusisitiza kuwa Sheikh Zakzaky anakaribia kupatwa na mshtuko wa moyo, kiharusi na kupofuka macho.

Hayo yamebainishwa mapema wiki hii na Katibu wa Jukwaa la Kielimu la Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Abdullahi Musa huko Abuja. Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imeweka wazi kuwa, mwanazuoni huyo yuko hatarini kupoteza kikamilifu uwezo wa kuona iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kuzuia kuzorota hali yake ya kiafya.

Taarifa ya harakati hiyo imeongeza kuwa, wiki moja baada ya kuchunguzwa hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky; utawala wa Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria umepuuza mapendekezo hayo na kumpeleka mwanazuoni huyo mgonjwa na mke wake katika jela yenye mazingira mabovu huko Kaduna ambako madaktari hawana hata suhula za matibabu.   

Sheikh Ibrahim Zakzaky amekuwa akisumbuliwa na matatizo mbalimbali ya kiafya kuanzia kukwama damu kuelekea katika moyo, matatizo ya neva, tatizo la kuona katika jicho lake lililosalia la kulia  na mengineyo. Aidha miongoni mwa mambo mengine kuna  kiwango kikubwa cha mada ya cadmium katika damu ya mwanazuoni huyo wa Nigeria.

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria pia imeeleza kuwa, mke wa Sheikh Zakzaky, Bi Zeenat naye anasumbuliwa na maradhi ya maumivu ya viungo (Arthritis); na madaktari wake wanasema kuwa alipaswa kutibiwa kwa kufanyiwa upasuaji tangu miaka miwili iliyopita. 

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imesema kuwa, Wanaigeria na taasisi za kimataifa zinapasa kuelewa kuwa, utawala wa Buhari unafahamu kikamilifu namna hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky inavyozidi kuwa mbaya siku baada ya siku; hata hivyo haijachukua hatua yoyote ya kutatua hali ya kiafya ya mwanazuoni huyo.

Vilevile imezihimiza jamuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu kupaza sauti ya kumtetea mwanazuoni huyo na kuilazimisha serikali ya Nigeria kumwachia huru.

342/