19 Agosti 2020 - 12:58
Kuendelea “mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa” mhimili wa siasa za uingiliaji mambo wa Marekani dhidi ya Venezuela

Katika hali ambayo hadi sasa siasa za “mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa” za Marekani dhidi ya Venezuela zimefeli na kugonga mwamba, Robert Charles O’Brein, mshauri wa usalama wa taifa wa White House amesisitiza kuwa, mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa utakuwa mhimili wa harakati za Washington dhidi ya Venezuela.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Sera za chuki na uhasama za Marekani dhidi ya mataifa ya Amerika ya Latini hususan katika kipindi cha uongozi wa Rais Donald Trump zimeshadidi na kushika kasi mno.

Ukweli wa mambo ni kuwa, katika miaka ya hivi karibuni Marekani imefanya hima na juhudi kubwa ili iweze kuziondoa madarakani tawala za mrengo wa kushoto katika mataifa hayo kwa kuviunga mkono na kuvisaidia vyama vya mrengo wa kulia na wapinzani katika nchi hizo. Mfano wa wazi ni mapinduzi baridi yaliyofanikiwa kumuondoa madarakani aliyekuwa Rais wa Bolivia Evo Morales, ambaye aliondolewa madarakani na wapinzani wa ndani waliokuwa wakipatiwa himaya na uungaji mkono wa serikali ya Washington.

Kimsingi ni kuwa, akthari ya nchi za Amerika ya Latini ambazo daima zimekuwa zikitazamwa na Marekani kama  uwanja na ukumbi wao wa kujifaragua na kueneza satuwa zake, katika miongo ya hivi karibuni zimefanikiwa kujinasua na hali hiyo na zikitegemea siasa zao zilizo dhidi ya ukoloni na kupigania uadilifu, zimeweza kufunga njia ya upenyaji ya Washington.

Venezuela na Cuba ni miongoni mwa mataifa hayo. Hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni kwa mara nyingine tena ubeberu wa Marekani kwa mataifa ya Amerika ya Latini umekuwa ukitiliwa mkazo na viongozi wa Washington. Marekani ikiwa na lengo la kustafidi na vyanzo vya utajiri vya mataifa hayo, kudhamini usalama wake na kuweza kushindana na mataifa kama China na Russia imekuwa ikifanya kila iwezalo iwe na satuwa na ushawishi katika eneo la Latin America hususan Venezuela na Cuba.

Gazeti la The Wall Street Journal limemnukuu mmoja wa viongozi wa Marekani akifichua malengo ya ikulu ya White House na kuandika: Juhudi za Trump za kuuangusha utawala wa Rais Nicolas Maduro huko Venezuela zinabainisha na kuweka wazi kuanza kwa stratijia mpya yenye lengo la kuifanya Washington iwe na nguvu zaidi katika Ukanda wa Amerika ya Latini.

Hata hivyo licha ya siasa hizo, katika miaka ya hivi karibuni Marekani imefeli na kugonga mwamba katika kufikia malengo yake hayo huko Venezuela na Cuba.

Katika miaka ya hivi karibuni, viongozi wa Washington wamefanya njama kubwa za kuipindua serikali ya Maduro na kumuweka madarakani kiongozi wa upinzani Juan Guaido ili waweze kufikia malengo yao ya kibeberu.

Ukweli wa mambo ni kuwa, Guaido kabla ya kutumiwa kama wenzo wa mageuzi nchini Venezuela ana jukumu pia la kutekeleza sehemu ya mipango mikubwa ya Trump katika eneo la Amerika ya Latini. Pamoja na hayo, hatua zote hizo za Marekani hadi sasa zimefeli na kugonga ukuta.

Katika miezi ya hivi karibuni baada ya kuongezeka ushirikiano wa kiuchumi wa Iran na Venezuela, kupelekwa meli za mafuta za Iran katika nchi hiyo kwa ajili ya kudhamini sehemu ya mahitaji ya nishati ya nchi hiyo na kadhalika kuzinduliwa duka kubwa la bidhaa za chakula, suhula za afya na viwanda lenye matawi mengi katika mji mkuu Caracas kwa mara nyingine tena jambo hilo limefelisha siasa za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa za Washington dhidi ya Venezuela.

Licha ya hayo, lakini viongozi wa Marekani wangali wanasisitiza juu ya kuendelezwa siasa za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya mataifa kama Venezuela ambapo sasa suala hilo linazungumziwa katika fremu ya hati ya kistratijia ya Marekani katika Amerika ya Latini hususan dhidi ya Venezuela na Cuba.

Kuhusiana na suala hilo, Daniel Larison mtaalamu wa masuala ya kisiasa ameandika: Marekani haina haki ya kuyawekea mashinikizo makubwa ya kiuchumi baadhi ya mataifa au kutaka kuziondoa madarakani tawala fulani kwa sababu tu ya kutaka kuyashinikiza ili yaipatie fursa na upendeleo zaidi Washington na hivyo kuwasababishia masaibu mamilioni ya wananchi wa nchi hizo.

Sisi tunapaswa kukubali na kukiri jambo hili kwamba, siasa za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa ni shambulio lisilostahiki, haramu na baya dhidi ya mataifa yote ambayo kimsingi hayajachukua hatua yoyote ile ya chuki na hasama dhidi ya Marekani na wala hayajatoa pigo kwa Washington.

Licha ya kuwa viongozi wa Marekani wana matumaini kwa kutumia ‘siasa za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa’ katika fremu ya stratijia mpya iliyoandaliwa, watafanikiwa kusukuma mbele gurudumu la siasazao za chuki na adawa dhidi ya eneo la Amerika ya Latini, lakini kwa kuzingatia mazingira na anga inayotawala hivi sasa, inaonekana kuwa, wamepata pigo jingine katika mipango na mikakati yao hiyo ya kisiasa.

342/