25 Agosti 2020 - 10:37
Safari ya Rafael Grossi mjini Tehran; fursa ya kujenga upya hali ya kuaminiana kati ya Iran na IAEA

Kwa kutegemea ripoti zilizotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ukaguzi mkali na wa kiwango cha juu zaidi katika historia ya wakala huo, ukiwemo ukaguzi kamili wa zaidi ya mara 30 kwa mwaka pamoja na ule wa kushtukiza kwa mujibu wa Protokali ya Nyongeza, umefanywa na wakaguzi wa IAEA katika vituo vya nyuklia vya Iran.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Kuhusiana na masuala hayo, Iran imekwenda mbali zaidi kwa kutekeleza hata mambo yaliyo nje ya wajibu wake; na licha ya kuhalifu ahadi na kutotekeleza wajibu wao baadhi ya pande husika katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, imeendelea kwa subira na uvumilivu kutekeleza majukumu yake na kuyaheshimu makubaliano hayo ya kimataifa.

Katika uwanja huo, ushirikiano ambao Iran imetoa kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ni wa kiwango cha kuridhisha, jambo ambalo wamelikiri hata wanaoyakosoa makubaliano ya JCPOA.

IAEA ilipaswa tokea awali iwe inachukua maamuzi yake kwa uhuru na bila ya upendeleo na kuhitimisha moja kwa moja usikilizaji wa tuhuma bandia na zisizo na hoja wala ushahidi wowote, zinazotolewa kuhusiana na shughuli za nyuklia za Iran; lakini mwenendo wake wa kusuasua juu ya suala hilo na kukubali kusukumwa na mashinikizo ya kisiasa kumekuwa kukiendelea mpaka kufikia kiwango cha kuharibu imani ya Iran kwa wakala huo wa atomiki. Hivi sasa Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Grossi yuko hapa mjini Tehran ili kufanya mazungumzo na maafisa wa Iran kuhusu masuala na masuulia ziliyonayo pande mbili za Jamhuri ya Kiislamu na IAEA.

Kwa mujibu wa sisitizo la maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, safari ya Mkurugenzi Mkuu huyo wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki haina uhusiano wowote na takwa la Marekani la kutaka kutekeleza "Utaratibu wa Papo kwa Papo wa Kurejesha Vikwazo", unaojulikana kitaalamu kama "Snapback Mechanism".

Kazem Gharib Abadi, mwakilishi wa kudumu wa Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao mjini Vienna, amesema, safari ya Grossi imefanyika kutokana na mwaliko uliotolewa na Iran na akasisitiza kwamba: "Tehran haitaruhusu watu wengine wawe waratibu wa uhusiano wa IAEA na Iran, hususan katika hali nyeti na hasasi ya hivi sasa."  

Gharib Abadi amekumbusha pia kwamba: "Suala muhimu kwa Iran ni kuona Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki unafanya kazi zake kwa kufuata misingi mitatu ya kutopendelea upande wowote, kuhakiki mambo kitaalamu na kuchukua maamuzi kwa uhuru; na katika masuala ya ukaguzi wa nyuklia pia kutokiuka misingi ya viwango vilivyowekwa na kutopindukia mpaka katika uhuru wake wa ufanyaji tathmini na utoaji data.

Nukta muhimu inayopasa kutiliwa mkazo katika safari ya Mkurugenzi Mkuu wa IAEA hapa mjini Tehran ni ripoti za mara kwa mara zilizotolewa na wakala huo kuthibitisha jinsi Iran inavyoendelea kutekeleza na kuheshimu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Ripoti hizo zinaonyesha kuwa, masuala yote ambayo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki inayawasilisha kwa Iran yanaweza kutatuliwa kupitia ushirikiano wa pande mbili, kwa sharti kwamba, matakwa ya IAEA yawe ni yenye kukubalika, na masuala yanayofanyiwa uhakiki, yawe yanahusiana na kadhia ya nyuklia. Kwa muktadha huo, kupuuza uangalizi na ukaguzi makini na wa mtawalia pamoja na ripoti chanya za wakala huo wa atomiki zilizotolewa kuhusiana na ushirikiano wa aina yake ambao ni nadra kushuhudiwa iliotoa Iran kwa IAEA, ni jambo lisilokubalika.

Nukta hii aliwahi kuiashiria pia balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika mashirika ya kimataifa yenye makao yao mjini Vienna katika barua kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki; na akamtaka Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo aziweke hadharani hatua na madai yasiyo na ukweli yanayotolewa na Marekani.

Hata hivyo jambo hilo halikufanyika; na Marekani imekuwa ikiendelea kutoa madai yake hayo hewa huku ikijaribu kuutia doa na kuonyesha kuwa hautoshi ushirikiano ambao Iran imekuwa ikitoa kwa IAEA.

Ni wazi kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inazielewa barabara haki zake za kisheria na wajibu wake katika kadhia ya nyuklia kulingana na taratibu za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na mkataba husika. Na ndiyo kusema kuwa haiwezi kukubali kuburuzwa kwa namna yoyote ile, wala kutekeleza mambo yasiyokubalika katika uwanja huo.

Kwa msingi huo, na kama tulivyoashiria katika anuani ya uchambuzi huu, safari hii ya kwanza rasmi kufanywa na Rafael Grossi hapa nchini akiwa Murugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ni fursa ya kujenga upya muamana na hali ya kuaminiana kati ya pande mbili.../

342/