19 Septemba 2020 - 09:18
Afrika Kusini: Tutaendelea kuliunga mkono taifa la Palestina

Naledi Pandor, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amesema katika mazungumzo ya simu aliyofanya jana Ijumaa na waziri mwenzake wa Palestina, Riyadh al Maliki, kwamba Pretoria itaendelea kuliunga mkono taifa la Palestina.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Pandor alisema katika mazungumzo hayo ya simu kwamba, Afrika Kusini inaunga mkono juhudi za kuundwa nchi huru ya Palestina, kuondoka Wazayuni katika ardhi wanazozikalia kwa mabavu kama ambavyo inaunga mkono kikamilifu malengo matukufu ya Palestina.

Vile vile amezungumzia hatua ya nchi mbili za Kiarabu za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Bahrain ya kutangaza uhusiano wao wa kawaida  na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema kuwa, baadhi ya nchi za Kiarabu zinafuata maelekezo kutoka kwa rais wa Marekani Donald Trump na zimekubali kuwa nyenzo za kumtumikia waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Jumanne iliyopita, mawaziri wa mambo ya nje wa Imarati na Bahrain walijipeleka kwa Donald Trump huko Marekani na kutia saini hati za kutangaza kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni tofauti kabisa na malengo ya wananchi wa Palestina.

Hadi hivi sasa ulimwengu mzima wa Kiislamu bali hata baadhi ya nchi zisizo za Waislamu, zinalaani kitendo hicho cha kisaliti cha Bahrain na Imarati.

Hatakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imeitaja hatua hiyo kuwa ni hatari kubwa na ni zawadi ya bure ambayo Imarati na Bahrain zimeupa utawala wa Kizayuni wa Israel.

342/