20 Oktoba 2020 - 11:57
Wasimamizi wa uchaguzi Tanzania watakiwa kufuata sheria

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania (NEC) imewaagiza wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya majimbo kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria ili kuepuka malalamiko yanayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Dkt. Wilson Charles, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC ametoa agizo hilo wakati anafungua mafunzo ya uchaguzi kwa wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo Kanda ya Ruvuma yenye Mikoa ya Njombe, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Iringa na Mbeya. Mafunzo hayo yamefanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.

Ameeleza kuwa, “Kama unavyoona Taifa letu sasa hivi kuna baadhi watu wanachokochoko sana,kwa hiyo mjitahidi kufanya kazi kwa kanuni na sheria za uchaguzi ili kuepuka shari ya watu hao’’

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa NEC amesema hadi sasa tume hiyo imeshatuma sehemu kubwa ya vifaa vya kufanikisha uchaguzi mkuu ambao unatarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu na kwamba vifaa hivyo vimekwishaanza kusambazwa na inatarajiwa hadi kufikia Oktoba 24 kila Halmashauri nchini itakuwa imepokea vifaa vyote vya uchaguzi.

Amewashauri wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo kuanza kuvipakua vifaa hivyo na kuvisambaza katika maeneo yote na kwamba wasisubiri hadi Oktoba 27.

Dkt Wilsom Charles ameongeza kuwa, “NEC katika uchaguzi wa mwaka huu tunataka kuwa tofauti ukilinganisha na mwaka 2015, kwanza Serikali imetuletea fedha zilizotokana na kodi za walipa kodi kwa wakati, hivi tunavyoongea zaidi ya shilingi bilioni 120 nimezishusha ngazi ya Halmashauri’’

342/