10 Desemba 2020 - 12:08
Safari ya Rais wa Misri nchini Ufaransa na kupamba moto upinzani na malalamiko dhidi yake

Safari ya hivi karibuni ya Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri nchini Ufaransa na mazungumzo aliyofanya na Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo vimeibua hasira na malalamiko ya waungaji mkono wa haki za binadamu.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Mamia ya wapinzani nchini Ufaransa walikusanyika mbele ya jengo la bunge la nchi hiyo, ambapo mbali na kulaani safari ya el Sisi huko Paris, walisisitiza pia kwamba rais huyo wa Misri ndiye "mhusika wa ukiukaji haki za binadamu na ukandamizaji wa kutisha dhidi ya wapinzani."

Abdel Fattah el Sisi amefanya safari ya kuitembelea Paris wakati misimamo yenye migongano iliyoonyeshwa na viongozi wa Ufaransa hasa katika miezi ya karibuni imekosolewa na kupigiwa kelele nyngi. Kwa miaka mingi viongozi wa Ufaransa wamekuwa wakijinasibu kuwa wanaheshimu uhuru na demokrasia na kujali haki za binadamu; na kwa sababu hiyo wakazishutumu na kuzilaumu nchi nyingi na hata kufika mbali zaidi kwa kuziwekea vikwazo au hata kuvunja uhusiano nazo baadhi ya nchi walizozitaja kuwa ni wakiukaji wa haki za binadamu; mfano hai wa karibuni kabisa ukiwa ni maandamano ya upinzani nchini Belarussia, ambapo nchi za Ulaya na hasa Ufaransa imechukua msimamo mkali wa kuiwekea vikwazo kadhaa nchi hiyo kwa kisingizio cha kukiuka haki za binadamu. Lakini misimamo hiyo imechukuliwa wakati katika miezi ya karibuni Waislamu wa Ufaransa wameandamwa na mashinikizo makali huku matukufu yao ya kidini yakitusiwa na kuvunjiwa heshima, lakini viongozi wa nchi hiyo na hasa rais Macron mwenyewe amesimama kidete kutetea maovu hayo kwa kisingizio cha kulinda uhuru na haki za binadamu.

Lakini hivi sasa katika kadhia ya Misri, licha ya rais wa nchi hiyo el Sisi kukosolewa vikali na taasisi na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu ndani na nje ya Misri kwa sababu ya ukandamizaji mkubwa na wa kutisha anaowafanyia wapinzani ikiwemo harakati ya Kiislamu ya Ikhwanul Muslimin, amepokewa kwa heshima zote na rais Emmanuel Macron alipowasili mjini Paris. Serikali ya Ufaransa si tu imeahidi kushirikiana na Misri, lakini pia imepanga kuiuzia silaha nchi hiyo, jambo ambalo limezidi kuzighadhibisha asasi za kutetea haki za binadamu.

Antoine Madeleine, afisa wa muungano wa kimataifa wa haki za binadamu anasema hivi kuhusiana na suala hilo: "ripoti zetu zinaonyesha ni kwa kiwango gani silaha za Ufaransa ilizouziwa Misri zimetumiwa na viongozi wa nchi hiyo kukandamiza wapinzani."

Kwa kweli si Ufaransa peke yake, bali nchi zingine kadhaa za Ulaya pia zina muamala wa kiundumakuwili katika kauli na vitendo vyao kuhusiana na haki za binadamu na utekelezaji wa nara na kaulimbiu za demokrasia. Kusema kweli maslahi ya kibiashara na kiuchumi ya nchi za Magharibi ndiyo yenye kipaumbele cha kwanza kuliko jambo lolote lile, kiasi kwamba katika miaka ya karibuni, viongozi wa nchi za Magharibi ikiwemo Marekani na Ufaransa wamekuwa kila mara wakitoa hakikisho la kuziuzia silaha tawala zinazojulikana kuwa ndio wakiukaji wakuu wa haki za binadamu. Kwa kutoa mfano tu, katika vita vya Yemen, Marekani na washirika wake zimeuza silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola kwa nchi zinazounda muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, ikiwemo Saudia yenyewe na Imarati. Hilo limefanyika wakati hadi sasa mashirika na taasisi nyingi za kimataifa, likiwemo shirika la kimataifa la Oxfam, Amnesty International na mengineyo, zimeshatoa miito mara kadhaa ya kuitaka Marekani na washirika wake zisimamishe uuzaji silaha kwa Saudia na pande zingine zinazohusika katika vita vya Yemen.

Kwa mujibu wa ripoti za taasisi za kimataifa ikiwemo ripoti iliyotolewa na "Taasisi ya Utafiti wa Amani ya Frankfurt" wakati vigezo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya vinataka wanaouziwa silaha wawe wanaheshimu za binadamu na sheria za kimataifa na kulinda amani na uthabiti, kila nchi moja ya Ulaya inaipiku nyingine katika kuziuzia silaha nchi ambazo ni wakiukaji wakubwa wa haki za binadamu.

Hivi sasa rais wa Ufaransa ameamua kumtandikia zulia jekundu Abdel Fattah el Sisi wakati kuna wafungwa wa kisiasa na kiitikadi zaidi ya 60,000 katika jela za Misri, huku mashirika na makundi mengi ya kutetea haki za binadamu yakitoa indhari kutokana na jinsi serikali ya Cairo inavyopuuza haki za wafungwa hao. Lakini pamoja na hayo inaonekana kwamba, mara hii Macron ameamua kuzitoa kafara hata kaulimbiu zake bandia na uigizaji wake wa kutetea haki za binadamu kwa ajili ya mikataba ya uuzaji silaha na maslahi ya kiuchumi yanayotokana na mauzo hayo. Kiasi kwamba bila ya haya wala kuona aibu yoyote ametangaza kinagaubaga kuwa, pamoja na kuwepo tatizo la haki za binadamu nchini Misri, Ufaransa itaiuzia tu nchi hiyo silaha.../

342/