27 Desemba 2020 - 12:06
"Kirusi cha corona cha Uingereza" chathibitika kuingia Ufaransa na Uhispania

Maafisa wa afya wa Ufaransa na Uhispania wamesema, aina mpya ya kirusi cha corona ambacho kiliripotiwa hivi karibuni kwa mara ya kwanza nchini Uingereza kimeshaingia pia katika nchi hizo mbili za Ulaya.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Wizara ya afya ya Ufaransa imetangaza kuwa, mtu wa kwanza aliyeambukizwa kirusi hicho cha Uingereza amegunduliwa nchini humo.

Mgonjwa huyo ni mwanamme Mfaransa anayeishi nchini Uingereza ambaye alirejea Ufaransa Desemba 19 akitokea mjini London.

Nayo wizara ya afya ya Uhispania imesema, imerekodi kesi ya kwanza nchini humo ya mtu aliye na kirusi cha corona cha Uingereza.

Inasemekana pia kwamba, katika nchi za Uswisi na Italia wamegunduliwa pia watu walioambukizwa spishi hiyo ya kirusi cha corona iliyogunduliwa nchini Uingereza.

Kituo cha kipimo cha hisabati cha maradhi ya kuambukiza chenye makao yake mjini London kimetangaza kuwa, spishi hiyo mpya ya kirusi cha corona ina uwezo wa kusambaa zaidi kwa asilimia 56 kulinganisha na spishi za kabla yake.

Wataalamu wa Shirika la Afya Duniani WHO tawi la Ulaya wameonya kuwa, endapo vizuizi na karantini za kiafya zilizowekwa zitaondolewa wakati wa mapumziko ya mwaka mpya, wakazi wa bara hilo wajiandae kukabiliana na maafa makubwa.

Nchi za Ulaya zimefunga mipaka yao ya pamoja na Uingereza na kuweka mpaka maalumu wa safari za kutoka na kuelekea huko, baada ya kugunduliwa aina mpya ya kirusi cha corona nchini humo...

342/