28 Januari 2021 - 13:00
Machafuko ya marufuku ya corona yashadidi Uholanzi; serikali yaomba msaada wa kijeshi kutoka nje

Machafuko ya kupinga marufuku ya corona yamekuwa makubwa nchini Uholanzi kiasi kwamba serikali ya nchi hiyo imeziomba Ujerumani na Ubelgiji ziisaidie kuzima ghasia hizo.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: machafuko yameenea katika miji mikubwa kama Rotterdam na Hilversum pamoja na Amsterdam, mji mkuu wa Uholanzi. Hadi sasa jeshi la polisi limeshawaweka kizuizini watu kwa mamia.

Polisi ya Uholanzi imeziomba Ujerumani na Ubelgiji zitume majeshi yao ya polisi ya kutuliza ghasia kwenda kuisaidia kudhibiti machafuko hayo.

Mameya wa miji mbalimbali ya Uholanzi pia wamewataka wananchi kushirikiana na polisi kama ambavyo serikali ya nchi hiyo imewaonya vikali watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuchochea wananchi kufanya fujo na maandamano.

Ghasia zimezuka katika miji mbalimbali ya Uholanzi na nchi kadhaa za barani Ulaya baada ya kuchukuliwa hatua kali ya kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19.

Hadi hivi sasa jeshi la polisi la Uholanzi limeshawatia nguvu mamia ya waandamanaji wanaopinga hatua hizo za kuukabili ugonjwa hatari wa corona.

Kwa upande wake, serikali ya Ureno nayo imeiomba jamii ya kimataifa iisaidie katika kupambana na ugonjwa wa COVID-19 na madhara yake mengi hasa ya kiuchumi yanayotokana na hatua zinazochukuliwa za kukabiliana nao.

Nchi za Ulaya kama vile Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na nchi nyingine kadhaa zimeamua kuweka sheria kali za kukabiliana na corona, ugonjwa ambao hadi hivi sasa hauna dawa na hakuna chanjo ya kuaminika ya kujikinga nao.

Hatua zinazochukuliwa kupambana na COVID-19 kwa kawaida zinakuwa na makali mengi hasa ya kiuchumi, masuala ambayo yamewachosha wananchi.

342/