12 Februari 2021 - 13:07
Corona ya Uingereza kuathiri dunia nzima

Afisa mmoja wa Uingereza amesema kuna uwezekano kwamba aina mpya ya kirusi cha corona kilichogunduliwa nchini humo ambacho kimekuwa maarufu kwa jina la "Corona ya Uingereza", kitaikumba dunia nzima.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Prof Sharon Peacock amesema kuwa, aina hiyo mpya ya kirusi cha corona inatia wasiwasi kwa sababu inadhoofisha kinga inayosababishwa na chanjo za corona. 

Prof. Peacock amesema kuwa, corona ya Uingereza ambayo sasa ndiyo iliyosambaa zaidi nchini humo yumkini ikashambulia maeneo yote ya dunia.

Ripoti zinasema aina hiyo mpya ya virusi vya corona vinasambaa kwa kasi kubwa katika meneo mbalimbali ya Uingereza hususan katika jiji la London. Maafisa wa afya wa Uingereza wanasema kuwa, aina hiyo mpya ya virusi vya corona inasambaa kwa kasi zaidi kwa asilimia 70 kuliko virusi vingine vya corona.

Kwa sasa Uingereza, baada ya Russia, ndiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watu walioambukizwa virusi vya corona barani Ulaya. 

Hivi karibuni wataalamu wa masuala ya tiba wa Uingereza waligundua aina nyingine mbili mpya za virusi vya corona nchini humo.

Mtaalamu mmoja wa virusi wa Uingereza ametahadharisha kuwa, nchi hiyo inaelekea kuwa kituo kikuu cha aina mpya ya virusi vya corona.

Takwimu zinaonyesha kuwa karibu watu milioni nne wameambukizwa virusi vya corona nchini Uingereza na 115,529 miongoni mwao wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo. 

342/