Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Kwa mujibu wa taarifa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa , Antonio Guterres kupitia taarifa iliyotolewa jijini New York, ameeleza kushtushwa na taarifa za kifo cha Rais John Magufuli na ametuma salamu za rambirambi kwa familia yake, seriali na wananchi wa Tanzania.
Kwa upande wake, kupitia mtandao wa Twitter Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani la Umoja wa Mataifa, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema, “salamu zangu za dhati za rambirambi kwa wananchi na serikali ya Tanzania kufuatia kifo cha Rais John Magufuli. Fikra zangu ziko na familia na taifa wakati huu wa kipindi kigumu.”
Kwingineko, kutoka Somalia, akiandika kwa lugha ya Kiswahili, Rais Mohammed Farmaajo amesema kwa niaba yake na kwa niaba ya serikali na taifa la Somalia, “ningependa kuwasilisha rambirambi zetu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumpoteza kiongozi Rais John Magufuli.
Tunalitakia Taifa zima na seriklai subra na utulivu katika kipindi hiki cha maombi na maombolezo.”
Wakati huo huo, Mama Samia Suluhu Hassan mapema leo asubuhi, saa nne asubuhi kwa majira ya Afrika Mashariki ameapishwa kuwa rais wa 6 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hafla ndogo iliyofanyika katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na marais wastaafu wa Tanzania na Zanzibar pamoja na viongozi wengine mbalimbali wa nchi hiyo.
Taarifa ya kifo cha Rais Magufuli, iilitangazwa Jumatano na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ambaye alisema Magufuli alifariki dunia kwa maradhi ya moyo baada ya kulazwa hospitalini tangu Machi 6.
Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, baada ya Rais Magufuli kufariki dunia, hakuna uchaguzi mwingine uliopaswa kufanyika katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki na badala yake, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameapishwa kuwa rais kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa miaka mitano.
342/