20 Machi 2021 - 14:22
Uturuki: Israel ni mkiukaji wa sheria za kimataifa

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imesema mpango wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kupora ardhi na kubomoa nyumba za Wapalestina unakanyaga wazi sheria za kimataifa.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Katika taarifa iliyonukuliwa na shirika la habari la Anadolu, wizara hiyo imebainisha kuwa, mpango huo wa utawala ghasibu wa Israel utakaowaacha bila makazi mamia ya Wapalestina hususan wakazi wa mashariki mwa Quds tukufu unaonesha azma ya Tel Aviv ya kuendelea kughusubu na kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina badala ya kufuata mkondo wa amani.

Taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imeongeza kuwa,  utawala huo pandikizi unachukua hatua hii wakati huu ambapo Palestina inajaribu kukabiliana na makali ya janga la corona.

Imeitaka jamii ya kimataifa kusimama na wananchi wa Palestina kupinga sera hiyo ya Wazayuni ya kunyakua ardhi za Wapalestina na kubomoa nyumba zao.

342/