Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza katika taarifa yake kwamba, mamilioni ya familia magharibi na katikati mwa Afrika zinakabiliwa na baa la njaa na kwamba, idadi hiyo imekuwa ikiongezeka siku baada ya siku.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya WFP imetanabahisha kwamba, kupanda kwa bei za bidhaa za chakula katika maeneo ambayo yanakabiliwa na vita na mapigano na kujitokeza athari mbaya za kiuchumi na kijamii kutokana na maradhi ya COVID-19 ni mambo mengine ambayo yamechangia kuongezeka idadi ya watu wanaotaabika kwa baa la njaa barani humo.
Tomson Phiri, msemaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) amesema kuwa, zaidi ya watu milioni 31 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kiwango ambacho ni kikubwa mno ikilinganishwa na huko nyuma.
Aidha amesema, kuongezeka machafuko katika eneo la Sahel Afrika huko Mali, Burkina Faso na Niger kumepelekea idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa kufikia milioni 6.5.
"Kupanda kwa bei ya bidhaa za chakula katika maeneo yote ya magharibi mwa Afrika kumeifanya idadi ya watu wanaopata taabu na mashaka makubwa kujidhaminia mahitaji yao ya chakula kuongezeka mno katika miezi ya hivi karibuni", amesisitiza msemaji huyo wa WFP.
342/