12 Desemba 2021 - 10:50
Kenya yaongeza kasi utoaji chanjo ya COVID

Wizara ya Afya ya Kenya imeazimia kuongeza kasi ya utoaji wa chanjo ya COVID-19 baada ya kupokea chanjo zaidi ya milioni 4.6 Jumatatu.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Waziri wa Afya wa Kenya Bw. Mutahi Kagwe amesema dozi milioni 4.3 za chanjo za Corona za Johnson & Johnson zimetolewa na Ujerumani, na dozi nyingine laki 4 za chanjo za AstraZeneca zimechangiwa na Argentina kupitia mpango wa COVAX. Amewahimiza wale wote ambao hawajapata chanjo kwenda kuchanja, akisema chanjo hizo za ziada ilizopokea Kenya zitaharakisha kampeni ya kuchanja watu kote nchini.

Takwimu kutoka Wizara ya Afya ya Kenya zimeonyesha kuwa hadi tarehe 3 mwezi huu, Kenya imekuwa na chanjo milioni 3.47. Hadi kufikia Jumatatu Kenya imewapatia watu milioni 7.68 chanjo za COVID-19 na milioni 3 kati yao wamepata dozi kamili ya chanjo. Kenya inapanga kuwapatia wananchi wake wasiopungua milioni 10 chanjo za COVID-19 ndani ya mwezi huu.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) Bw. John Nkengasong ametangaza kuwa hadi sasa nchi 11 za Afrika zimeripoti wagonjwa wa COVID-19 wenye virusi vya Omicron, zikiwemo Afrika Kusini, Botswana, Nigeria, Ghana, Uganda, Zambia, Senegal, Tunisia, Msumbiji, Namibia na Zimbabwe.

Umoja wa Afrika (AU) umeonya kwamba marufuku ya kusafiri na kuingia inayohusiana na kuibuka kwa virusi vya Omicron inazuia usafirishaji huru wa watu na bidhaa, na kuleta athari za haraka na kubwa kwa nchi za Afrika.

Umoja wa Afrika wenye wanachama 55 ulitoa wito wa kuondolewa haraka marufuku ya kusafiri iliyowekwa katika nchi za kusini mwa Afrika kufuatia kugunduliwa kwa Omicron.

Ushahidi uliopo, ambao unasisitiza kuenea na kusambaa kwa virusi vya Omicron duniani na kwenye jamii, hauna mashiko kwenye upande wa marufuku hiyo ya kusafiri iliyowekewa nchi za Kusini mwa Afrika.



342/