Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Ismail Hania Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ambapo sambamba na kumpa pongezi kiongozi huyo kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuanzishwa harakati ya Hamas amebainisha kwamba, mataifa machache ya Kiarabu ambayo yamechukua mkondo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel yamefanya jambo ambalo ni kinyume kabisa na usalama na maslahi ya eneo hili na Umma wa Kiislamu.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS iko mstari wa mbele katika harakati za kuikomboa Baitul-Muqaddas na kwamba, hii leo muqawama ni mhimili muhimu katika kupigania haki za kihistoria za wananchi wa Palestina.
Abdollahian amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuunga mkono muqawama na harakati za ukombozi za wananchi wa Palestina.
Kwa upande wake Ismail Hania, Mkuu wa Ofisi ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amelaani hatua ya baadhi ya mataifa ya Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kueleza bayana kwamba, hatua hiyo ni utendaji wa Kimarekani-Kizayuni.
342/