17 Desemba 2021 - 19:15
Homa ya Lassa yaua watu 80 chini Nigeria

Jumla ya watu 80 wameripotiwa kupoteza maisha kwa homa ya Lassa katika sehemu mbalimbali za Nigeria. Hayo yamesemwa na Kituo cha Kudhibiti Magonjwa ya Kuambukiza cha nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika (NCDC).

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Kwa mujibu wa NCDC, mbali na kufariki dunia watu hao 80 tangu mwanzoni mwa mwaka huu, idadi ya kesi za homa ya Lassa zilizosajiliwa nchini Nigeria kukanzia mwezi Januari hadi Disemba 8 mwaka huu ni 434 katika majimbo 17 ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Homa ya Lassa huenea kwa wanadamu kupitia chakula na vifaa vya ndani ya nyumba vilivyochafuliwa na kinyesi pamoja na mikojo ya wadudu kama panya n.k.

Ugonjwa wa homa ya Lassa ulishuhudiwa kwa mara ya kwanza nchini Nigeria mwaka 1969 katika mji wa Lassa na ndio maana ulipewa jina la mji huo. Ugonjwa huo unashabihiana sana na ule wa Ebola na Marbug.

Mwaka 2019, serikali ya Nigeria ilitangaza kuzuka tena ugonjwa wa homa ya Lassa nchini humo ambapo katika kipindi cha mwaka huo wa 2019 karibu watu 170 walipoteza maisha kutokana na homa hiyo hatari.

Mwezi Februari mwaka jana 2020 pia, kesi ya kwanza ya mripuko wa homa ya Lassa ilithibitishwa katika mji mkuu wa kibiashara wa Nigeria, Lagos. Serikali ya jimbo la Lagos iliandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter ikisema kuwa, "mtu aliyeathiriwa ametengwa katika chumba mahsusi hospitalini.

Kituo hicho cha Kudhibiti Magonjwa ya Kuambukiza nchini Nigeria (NCDC) kiliripoti pia kuwa, idadi ya watu waliopoteza maisha nchini humo kutokana na mripuko mpya wa homa ya Lassa hadi wakati huo ilikuwa imeongezeka na kufikia 103.

342/