Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Saeed Khatibzadeh amejibu propaganda hizo chafu za baadhi ya maafisa wa Marekani na Ulaya kuhusiana na majaribio ya kurusha angani roketi ya kubeba satalaiti ya Simorgh akisema kuwa, maendeleo ya kisayansi na kitafiti ikiwa ni pamoja na katika nyanja za masuala ya anga, ni haki ya taifa la Iran na kwamba, matamshi hayo hayatadhoofisha azma ya watu wa Iran ya kupiga hatua zaidi za maendeleo katika uwanja huo. Khatibzadeh amesema kuwa hakuna azimio lolote linaloizuia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa na miradi ya utafiti wa masuala ya anga na kufanya majaribio yanayohusiana na sekta hiyo yakiwemo ya satelaiti; hivyo basi kunukuu azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la UN ni upotoshaji na madai yasio na msingi wowote.
Ni dhahiri kuwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina haki ya kutumia teknolojia ya amani katika maendeleo yake ya kisayansi na utafiti.
Itakumbukwa kuwa, Wizara ya Ulinzi ya Iran ilitangaza Alkhamisi iliyopita kuwa imerusha kwa mafanikio roketi ya Simorgh inayotumiwa kupeleka satalaiti katika anga za mbali. Kuhusu majukumu ya roketi la Simorgh, Msemaji wa Timu ya Anga za Mbali ya Wizara ya Ulinzi ya Iran Sayyid Ahmad Hosseini amesema, sehemu zote zilizohusika na urushaji wa roketi hiyo ya majaribio zimefanya kazi zake vizuri na kufanikiwa kufikia lengo lililokusudiwa.
Suala la kutengeneza maroketi yenye nguvu za kubeba satalaiti kubwa zaidi katika masafa ya mbali zaidi lilipata nguvu na kuwa moja ya ajenda kuu za wizara hiyo baada ya Iran kupata mafanikio katika kurusha angani satalaiti ndogo kwa kutumia maroketi ya Safir na Ghasedak. Uwezo huo unatokana na maendeleo ya kisayansi na unasisitiza kuwa taifa la Iran linastahiki maendeleo na ustawi.
Hatua za kisayansi na kiutafiti za Iran katika masuala ya anga za mbali zinaonyesha kuwa, ari na uwezo wa wanaviwanda na wanasayansi wa Iran ni mkubwa kiasi kwamba matamshi na vikwazo vya nchi za Magharibi haviwezi kukwamisha ustawi na maendeleo ya Iran. Nemat Hassani, profesa msaidizi na mtafiti katika Chuo Kikuu cha Shahid Beheshti, anaashiria umuhimu wa maendeleo ya kisayansi na kusema: Teknolojia ya masuala ya anga ni mojawapo ya nyenzo muhimu zaidi za usimamizi wa masuala ya ustawi.
Kazi kuu ya teknolojia ya kurusha satalaiti anga za mbali ni kukusanya taarifa zinazohitajika kwa ajili ya kutathmini na kufuatilia hatari za maafa ya kimaumbile kupitia vituo vya masuala ya anga. Hivi sasa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa kubuni mfumo kamili wa teknolojia ya anga kutokana na juhudi kubwa za Shirika la Masuala ya Anga la Iran licha ya mashinikizo na vikwazo vyote vya kisayansi vya nchi za Magharibi. Baada ya kutengeneza satalaiti, kuituma anga za mbali na kupokea data na taarifa zake, Iran imenufaika na teknolojia hiyo kwa ajili ya utafiti ya kisayansi na mipango ya maendeleo, na sasa teknolojia ya anga za juu imekuwa jambo linaodhibitiwa na wasomi wa ndani ya nchi. Roketi ya kubeba satalaiti ya Simorgh ya Iran ina uwezo wa kurusha satalaiti zenye uzito wa kilo 250 katika mzunguko wa kilomita 500 wa ardhi.
Kwa kurusha satalaiti anga za mbali na kuingia katika kundi la nchi zenye teknolojia ya makombora na maroketi ya kupeleka satalaiti angani, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonyesha kuwa ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani katika sayansi ya masuala ya anga. Kwa sasa, ni chini ya nchi 10 tu duniani, ikiwemo Iran, zenye uwezo wa kujenga vituo na taasisi za kurushia satalaiti anga za mbali ambako kunahitaji uwezo na teknolojia ya hali ya juu.
Katika miaka yote iliyopita maadui wamejaribu kuizuia Jamhuri ya Kiislamu kupata teknolojia hizo za hali ya juu kwa mashinikizo na vikwazo; lakini maafisa wa serikali na wanasayansi wamezuia njama hizo kwa kutetea haki za nyuklia na kisayansi za watu wa Iran.
Kurushwa kwa mafanikio roketi ya kutuma satalaiti angani ya "Simorgh" kwa mara nyingine tena kumeonyesha kuwa, shughuli za kisayansi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sio tu kwamba hazijasimama, bali zinaendelea kushika kasi kwa mafanikio zaidi. Kwa msingi huo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, Iran haitasubiri maoni ya baadhi ya nchi zinazojaribu kulazimisha maoni na mitazamo yao, na harakati inayokwenda kwa kasi kubwa ya maendeleo ya kisayansi hapa nchini haitakuwa rehani na kukwamishwa na uzushi wa madola ya wageni.
/342