Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Mji wa Mariupol umeshambuliwa pakubwa huko Ukraine ukilinganisha na miji mingine ya nchi hiyo tangu Russia ianzishe mashambulizi dhidi ya Ukraine Februari 24 mwaka huu. Wakazi laki nne wa mji huo wako katika mkwamo kutokana na kuendelea mapigano katika mitaa ya kandokando ya mji huo.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa, Iryna Vereshchuk, Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine amejibu ombi la Russia la kujisalimisha mji wa Mariupol na kueleza kuwa: hakuna mjadala kuhusu kujisalimisha au suala la kuweka chini silaha. "Huko nyuma tuliwaeleza Russia kuhusu suala hilo", amesema Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine.
Russia imewataka wanajeshi wa Ukraine walioko katika mji wa Mariupol waweke chini silaha zao ili wanajeshi hao waweze kutoka salama salimini katika mji huo; na pia imewataka wanajeshi hao wafungue vivuko vinavyotumika kwa ajili ya masuala ya kibinadamu huko Mariupol kuanzia saa nne asubuhi kwa wakati wa Moscow; ombi ambalo limekataliwa na serikali ya Kyiv.
Hii ni katika hali ambayo Naibu Waziri Mkuu wa Ukraine awali alieleza kuwa zaidi ya watu elfu saba wameondolewa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kupitia vivuko salama tangu Jumapili iliyopita; ambapo zaidi ya nusu ya raia hao ni wakazi wa mji wa Mariupol. Amesema, serikali ya Ukraine jana Jumatatu ilipanga kutuma mabasi karibu 50 huko Mariupol kwa ajili ya kuwahamisha raia wengine zaidi. Wakati huo huo mashirika mbalimbali ya habari ya Russia yameripoti kuwa, mabasi kadhaa katika siku za karibuni yameshuhudiwa yakiwa yamewabeba mamia ya wakimbizi kutoka Mariupol kuelekea Russia.
Moscow kwa upande wake imesisitiza mara kadhaa kwamba haina lengo la kuikalia kwa mabavu Ukraine.
342/