31 Machi 2022 - 17:05
Guterres: Watu bilioni 2 wanaishi katika maeneo yaliyoathiriwa na machafuko

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema dunia inakabiliwa na idadi kubwa zaidi ya mapigano makali tangu mwaka 1945, wakati Vita vya Pili vya Dunia vilipomalizika.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Antonio Guterres ameiambia Tume ya Amani ya Umoja wa Mataifa kwamba robo ya wanaadamu - sawa na watu bilioni mbili -, sasa wanaishi katika maeneo yenye migogoro. 

Akiashiria migogoro ya Yemen, Syria, Myanmar, Sudan, Haiti, ukanda wa Sahel barani Afrika na Ukraine, Guterres amesema majanga hayo yanayumbisha misingi ya mfumo wa kimataifa, yanavuka mipaka na kupandisha juu bei za chakula, nishati na mbolea; suala mabalo ni janga kubwa kwa nchi zinazoendelea.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, watu milioni 84 walilazimika kukimbia makazi yao mwaka jana kutokana na migogoro, ghasia na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Idadi hiyo haijumuishi vita vya Ukraine, ambavyo kwa mujibu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, hadi sasa vimewalazimisha watu milioni nne kukimbia nchi hiyo na milioni 6.5 kuwa wakimbizi wa ndani. 

Kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa, takriban watu milioni 274 watahitaji msaada wa kibinadamu mwaka huu wa 2022.

Takwimu za Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu zinaonesha kuwa, makadirio hayo yanawakilisha ongezeko la asilimia 17 kutoka 2021 na yatagharimu dola bilioni 41 kwa ajili ya watu milioni 183 wanaohitaji misaada ya kibinadamu.

342/