9 Aprili 2022 - 14:35
Uchaguzi wa bunge wafanyika Gambia

Wananchi wa Gambia wamepiga kura kuchagua Bunge jipya la Kitaifa katika uchaguzi unaolenga kuimarisha demokrasia changa nchini humo.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Zoezi la upigaji kura lilianza saa nne asubuhi (08:00 GMT) na lilitazamiwa kufungwa saa kumi na moja jioni (17:00 GMT) ambapo wananchi wanawachagua wabunge 53 kwa ajili ya kipindi cha miaka mitano. Matokeo yanatarajiwa Jumapili ijayo.

Takriban waangalizi 40 wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) wametumwa katika mikoa saba ya nchi hiyo ili kufuatilia mchakato wa uchaguzi.

Rais Adama Barrow wa Gambia aliingia madarakani mwaka wa 2017 baada ya kushinda uchaguzi wa rais ulioashiria mwisho wa utawala wa Yahya Jammeh ambaye alilazimika kwenda uhamishoni.

Mwezi Disemba mwaka jana, Barrow alichaguliwa tena kuwa rais katika kile kilichoonekana kwa kiasi kikubwa kama mtihani wa utulivu wa demokrasia katika nchi hiyo ndogo ya Magharibi mwa Afrika.

Weledi wa mambo wanasema kuna uwezekano kwamba Rais Barrow atalidhibiti Bunge kwa kuchaguliwa wabunge wengi wanaomuunga mkono.

Barrow anakabiliwa na upinzani uliogawanyika na usio na umaarufu.

Wataalamu pia wanatabiri idadi ndogo ya washiriki katika uchaguzi huo wa leo Jumamosi kutokana na hali ya kutojali na kupoteza matumaini wananchi kwa sababu ya hali mbaya ya kiuchumi.

Gambia ni miongoni mwa nchi 15 zenye maendeleo duni zaidi duniani, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Utalii, uti wa mgongo wa uchumi wa nchi, ulivurugwa na janga la corona, na kuweka hatarini ajira za watu karibu 140,000 wanaohusika katika sekta hiyo katika nchi ambayo ina idadi ya watu takribani milioni 2.4.

342/