Shirin Abu Aqleh alikuwa ripota wa Kipalestina wa Kanali ya al-Jazeera ya Qatar ambaye aliuawa shahidi na mwanajeshi wa Israel mnamo Mei 11, 2022 huko Jenin, katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Wapalestina pamoja na televisheni ya al-Jazeera wanasisitiza kuwa mauaji hayo yalitekelezwa kwa makusudi lakini jeshi la Israel, mbali na kukiri kuwa yalifanywa na mwanajeshi wake, lakini linadai kuwa yalifanyika bila kukusudia.
Mauaji ya raia hususan waandishi wa habari katika makabiliano ya kijeshi kati ya Wazayuni na Wapalestina si tukio lisilo la kawaida wala la kipekee, bali ni mwenendo wa kila siku na uliopangwa. Akiwa raia wa Palestina na mwandishi wa habari, Shirin Abu Aqla alilengwa na kuuawa kwa makusudi na wanajeshi wa Kizayuni. Tangu mwaka 2000, waandishi wa habari 45 wameuawa shahidi na majeshi ya Kizayuni, na bila shaka mauaji ya Shirin Abu Aqla hayatakuwa ya mwisho.
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imeombwa kushughulikia haraka uhalifu huo kwa sababu mahakama hiyo mnamo Februari 2021, katika taarifa, ilitambua mamlaka yake ya kushughulikia uhalifu ambao unafanyika katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. Kwa msingi huo, mahakama hiyo sasa ina jukumu la kisheria la kushughulikia haraka mauaji ya Shirin Abu Aqla. Suala jingine ni kuwa, kuuawa shahidi Shirin Abu Aqla kutaiwezesha Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kufuatilia kwa umakini zaidi uamuzi ilioutoa mwaka jana wa kuingia na kuchunguza jinai za Wazayuni katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu. Wataalamu wa sheria wa Umoja wa Mataifa awali walitangaza katika taarifa kwamba kuuawa kwa mwandishi wa habari wa Kipalestina Shirin Abu Aqla wa al-Jazeera akiwa amevalia sare ya mwandishi wa habari ni sawa na uhalifu wa kivita.
Jambo jingine kuhusu kupelekwa kesi hiyo kwenye Mahakama ya Jinai ICC ni kwamba kujeruhiwa Ali Sammoudi, mfanyakazi mwenza wa mwandishi wa Abu Aqla, na kulengwa Shadhi Hanaisha, mwenzao mwingine, Mei 11 huko Jenin, pia kumejumuishwa katika kesi ya Shirin Abu Aqla na kesi mbili hizo pia zimetikiwa zichunguzwe haraka iwezekanavyo. Kwa hiyo, kesi hiyo ina mashahidi wawili walio hai katika mahakama hiyo ya kimataifa ya jinai.
Kupelekwa kesi hiyo katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kumefanyika katika hali ambayo utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake wa kigeni hususan wa Magharibi walitumia mashinikizo mengi makali ili kuzuia kesi hiyo isipelekwe mahakamani. Hivyo kufikishwa kesi hiyo mahakamani ni kushindwa kwa utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake na vilevile ni ushindi wa kisheria kwa Wapalestina. Ndio maana mwaka jana Wazayuni wakapinga vikali kutambuliwa mamlaka ya mahakama hiyo kushughulikia matukio ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Kwa mujibu wa sheria zake, mahakama ya ICC inaweza kumuadhibu mtu yeyote aliyetekeleza jinai ya mauaji ya Shirin Abu Aqla na pia kuliadhibu pia jeshi la Israel kwa kuwa mwanajeshi aliyehusika na jinai hiyo ni mwanachama wake na tayari jeshi hilo hapo awali lilikuwa limekiri kuhusika askari huyo na uhalifu huo. Mahakama hiyo ina mamlaka ya kuadhibu watu binafsi na taasisi, na hata kinga ya watu binafsi haiwezi kuwa kikwazo mbele ya adhabu hiyo.
Pamoja na hayo, hata kama kupelekwa kesi hiyo mahakamani kunahesabiwa kuwa ni ushindi wa kisheria kwa Wapalestina, ni wazi kuwa hata hatua za kisheria za mahakama hiyo haziwezi kuzuia kurudiwa kwa jinai hizo za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wasio na hatia. Hii ni kwa sababu kwa upande mmoja utambulisho wa asili wa utawala huo ni kutenda jinai, na kwa upande mwingine madola ya Magharibi hususan Marekani yanauunga mkono kwa dhati. Bila shaka ni uungaji mkono huo ndio unaufanya utawala huo wa kigaidi uweze kukwepa adhabu na mkondo wa sheria za kimataifa.
342/