17 Oktoba 2022 - 19:37
Moscow yasisitiza kuendelea na vita huko Ukraine

Msemaji wa Rais wa Russia amesisitiza kuwa, oparesheni maalumu itaendelea huko Ukraine hadi mwisho licha ya Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato) kuingia vitani nchini humo.

Nchi wanachama wa Nato khususan Marekani, Uingereza na Ujerumani mbali na kuipatia Ukraine silaha na zana za kijeshi zimeingilia kati mgogoro wa nchi hiyo kwa kuipatia Kiev taarifa za kijasusi. 

Moscow imezitahadharisha nchi hizo mara nyingi kwamba misaada inayotoa kwa Ukraine inavifanya vita vya Ukraine vidumu kwa muda mrefu na kuuawa watu wengi.   

Dmitry Peskov Msemaji wa Rais wa Russia aidha ameeleza kuwa, ni wazi kuwa Nato imeingia vitani kikamilifu uko Ukraine lakini hatua hiyo haiathiri kivyovyote malengo ya Shirikisho la Russia. Amesema Moscow itaendelea na oparesheni zake maalumu huko Ukraine hadi mwisho.  

Msemaji wa Kremlin ameongeza kuwa, uingiliaji wa Nato katika mapigano huko Ukraine unaifanya hali ya mambo kuwa mbaya zaidi lakini uwezo wa Russia unatoa mwanya kwa nchi hiyo kuendelea na oparesheni zake maalumu dhidi ya Ukraine. 

Jens Stoltenberg Katibu Mkuu wa Nato aliwahi kusema, "ushindi wa Russia katika vita hivyo si pigo kubwa kwa raia wa Ukraine pekee bali litakuwa pigo na kitendo cha hatari kwetu sote."