31 Oktoba 2022 - 19:46
Lula ashinda uchaguzi wa Rais Brazil baada ya kumuangusha Bolsonaro

Rais wa zamani wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva Jumapili alimshinda Jair Bolsonaro katika uchaguzi ambao unaashiria kurejea madarakani kwa kishindo kiongozi huyo wa mrengo wa kushoto.

Lula da Silva alikuwa na asilimia 50.8 ya kura ikilinganishwa na asilimia 49.2 ya kura za Bolsonaro baada ya asilimia 99.1 ya kura kuhesabiwa na kwa msingi huo Mahakama ya Juu ya Uchaguzi ikasema ilitosha kumtangaza mshindi.

Ushindi wa da  Silva umetajwa kuwa ni kemeo kwa sera za kufurutu ada za mrengo wa kulia ambazo Bolsonaro alikuwa akitekeleza.

Utawala wa Bolsonaro umelaumiwa kwa kuvuruga uchumi wa Brazi na pia usimamizi mbovu wa sekta ya afya jambo ambalo lilipelekea nchi hiyo kuongoza duniani kwa idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na janga la COVID-19.

Lula da Silva amesema atarejesha sera za kustawisha ukuaji wa uchumi ambazo zilisaidia kuwaondoa mamilioni ya watu kutoka kwenye umaskini wakati alipoitawala Brazili kutoka 2003 hadi 2010. Pia ameahidi kupambana na uharibifu wa msitu wa Amazon, ambao ni muhimu katika kuzuia athari mbaya za mabadiliko ya tabia nchi duniani. 

Lula da Silva (kulia) na Jair Bolsonaro

Ushindi wa Lula da Silva umetajwa kuwa ni "wimbi la waridi" katika ukanda wa Amerika ya Kusini, baada ya ushindi wa kihistoria wa mirengo ya kushoto nchini Colombia na Chile.

Lula da Silva ni kiongozi wa zamani wa chama cha wafanyakazi na alizaliwa katika umaskini. Aliongoza mgomo dhidi ya serikali ya kijeshi ya Brazil katika miaka ya 1970.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Lula da Silva amesema Brazil sasa imerejea tena katika uga wa kimataifa na haitakuwa nchi iliyotengwa. Rais mpya wa Brazil ataingia rasmi ofisini Januari 1.

342/