15 Desemba 2022 - 19:41
Kan'ani Chafi: Azimio la Marekani dhidi ya Iran katika kikao cha ECOSOC halina hadhi ya kisheria

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali azimio lisilo na ridhaa ya wote la Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kikao cha Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa (ECOSOC) na kulitaja kuwa ni hatua ya kisiasa, iliyokosa hadhi ya kisheria, iliyo kinyume na Hati ya Umoja wa Mataifa na yenye kuanzisha utaratibu mbaya katika taasisi hiyo ya kimataifa.

Uanachama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hadhi ya Wanawake ulimalizika Jumatano usiku kufuatia ombi lililo kinyume na sheria la Marekani la kutaka kuhitimishwa uanachama huo kwa kutegemea madai yasiyo na msingi na ya hoja bandia na kwa kutumia simulizi za kubuni na zinazopingana na dhati na Hati ya Umoja wa Mataifa.Azimio hilo lilipitishwa kwa kura 29 za ndiyo, kura nane zilizopinga na 16 za wajumbe walioamua kutopiga kura.Bolivia, China, Kazakhstan, Nicaragua, Nigeria, Oman, Russia na Zimbabwe zilipiga kura ya kupinga kufutwa uanachama wa Iran katika Kamati ya Hadhi ya Wanawake.

Kamati ya Hali ya Wanawake ni moja ya mihimili ya Baraza la Umoja wa Mataifa la Kijamii na Kiuchumi (ECOSOC). Azimio la kufuta ushiriki wa Iran katika kamati hiyo liliwasilishwa na serikali ya Marekani ikiwa ni katika kuendeleza mashinikizo ya kimataifa dhidi ya Iran kwa lengo la kuunga mkono machafuko yaliyozuka hapa nchini.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Nasser Kan'ani Chafi amesema Iran imekuwa mwanachama wa Kamati ya Hadhi ya Wanawake kwa mihula miwili katika kipindi cha miaka 10 iliyopita (tangu 2011), na wakati wa uchaguzi wa mwaka jana, ilichaguliwa kuwa mjumbe kwa mara ya tatu kwa kura nyingi zaidi ambazo ni 43 kati ya 54 za wanachama wa Ecosoc na akaongeza kuwa: hatua hii ya kiuadui ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni jaribio la Washington la kulazimisha matakwa yake ya kisiasa ya upande mmoja na kupuuza utaratibu wa uchaguzi katika taasisi za kimataifa.Msemaji wa vyombo vya kidiplomasia vya Iran amebainisha kuwa: kumnyima nafasi yake mjumbe halali na wa kisheria wa Kamati ya Hadhi ya Wanawake ni uzushi wa kisiasa, unaochafua itibari ya taasisi hiyo ya kimataifa na pia ni kuanzisha utaratibu wa kuchukua hatua za upande mmoja zitakazokuja kuzitumia vibaya taasisi za kimataifa katika siku za usoni. Aidha amesema, ni kichekesho kuona utawala bandia wa Israel wenye rekodi chafu ya jinai zilizoratibiwa dhidi ya taifa madhulumu la Palestina unakuwa mjumbe wa Kamati ya Hadhi ya Wanawake kwa uungaji mkono wa Marekani na vibaraka wake.../


342/