Tamko hilo la IOM limetolewa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Wahamiaji ambayo inaadhimishwa leo tarehe 18 Desemba
Katika siku hii ya wahamiaji, IOM imesambaza video mbalimbali za wahamiaji ambapo katika moja ya video hizo mhamiaj immoja anasikika akisema, "Mimi ni mhamiaji," akijinadi kwa ujasiri huku mwingine akieleza kuwa mhamiaji ni mtu kama mwanadamu mwingine yeyote ambaye amejikuta haishi kwenye nchi aliyozaliwa.
Kwa mujibu wa IOM kuna sababu lukuki zinazowalazimisha watu kufungasha virago na kwenda katika nchi nyingine, sababu kama vile vita, usalama, mabadiliko ya tabianchi, njaa, na hata kusaka mustakbali bora na wengi wanacho cha kuchangia katika jamii wanakokwenda. Hata hivyo mara nyingi kama anavyosema Antonio Vitorino Mkurugenzi Mkuu wa IOM katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya wahamiaji mchango wao hauonekani wala kuthaminiwa.
Amesema wahamiaji wamekuwa msingi wa maendeleo na hatua zilizopigwa, na wametajirisha jamii na nchi tangu enzi za kale. Afisa huyo wa IOM amebainisha kuwa pamoja na kuwa wahamiaji wana mchango mkubwa, lakini ndio watu ambao mara nyingi wanateseka, wanakwama, kunyanyaswa, kudhalilishwa na kubaguliwa.
Vitorino ameongeza kuwa uhamiaji haukuanza jana wala leo, umekuwa ni moja ya hulka za kale sana hivyo amesihi kutoruhusu kuingizwa siasa, chuki dhidi ya wageni na mambo mengine kama hayo kwenye suala la uhamiaji.
Hali kadhalika ameongeza kuwa, “Watu wanahama kwa sababu nyingi na kwa njia mbalimbali, lakini bila kujali kilichowafanya watu kuhama, haki zao, utu wao lazima ziheshimiwe na mchango wao utambuliwe.”
Amehitimisha ujumbe wake kwa kusisitiza kwamba “jambo la msingi kabisa wahamiaji kwanza ni binadamu, watu, ndugu, majirani na viongozi na hivyo dunia inapaswa kuwasaidia na sio kuwabagua.”
Maudhui ya mwaka huu ya siku ya wahamiaji ni kuhimiza dunia kutafakari na kutambua mchango muhimu wa wahamiaji.