21 Desemba 2022 - 21:05
Mazungumzo ya Josep Borrell na Amir-Abdollahian nchini Jordan; msimamo baridi wa Umoja wa Ulaya

Jumanne ya jana tarehe 20 Disemba, Waziri wa Mashauri ya Kiigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya pambizoni mwa mkutano wa Baghdad-2 uliofanyika katika mji mkuu wa Jordan, Amman.

Hussein Amir-Abdollahian na Joseph Borrel walitumia fursa hiyo ya mazungumzo baina yao kwa ajili ya kubadilishana mawazo kuhusiana na masuala muhimu yaliyoko katika ajenda ya Iran na Umoja wa Ulaya hususan mazingira yanayotawala katika mazungumzo ya nyuklia ya Vienna Austria.

Abdollahian ameeleza katika mazungumzo hayo juu ya utayari wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kukusanya nukta na mitazanmo ya mazungumzo ya Vienna kwa mujibu wa kifurushi cha mapendekezo ya mazungumzo ambacho ni matokeo ya mazungumzo magumu ya miezi kadhaa. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameunasihi upande wa pili katika mazungumzo ya nyuklia ujiepushe na matashi ya kisiasa na badala yake uchukue maamuzi kwa kuzingatia uhalisia wa mambo.

Kwa upande wake Josep Borrel, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya amebainisha misimamo na utendaji wa umoja huo kuhusiana na Iran katika miezi ya hivi karibuni, kadhia ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kueleza kwamba, mazungumzo ya nyuklia ni kadhia kando kabisa na masuala mengine baina ya pande mbili na kusisitiza juu ya kuweko azma imara kwa ajili ya kufikia natija mazungumzo ya Vienna. Borrell ameandika ujumbe katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kwamba: Tumekubaliana kwamba, kuna haja ya kudumisha mawasiliano na kuhuisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kwa msingi wa mazungumzo ya Vienna.

Inaonekana kuwa, kubadilika msimamo wa Umoja wa Ulaya kuhusiana na kuhuisha mazungumzo ya nyuklia ya Vienna chimbuko lake ni kutulia hali ya mambo nchini Iran, kufikia tamati fujo na vurugu na kukata tamaa Brussels na suala la kuendelea machafuko hapa nchini yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya watu waliohadaiwa wakitumia kisingizio cha kifo cha Mahsa Amini.