2 Machi 2023 - 14:23
China yapendekeza mpango wa amani wa Ukraine

Mwaka mmoja umepita tangu kuzuka vita nchini Ukraine na matarajio ya kumalizika vita hivyo bado ni ya kukatisha tamaa.

Badala ya kuunga mkono mazungumzo na suluhu ya amani kwa mzozo huo, nchi za Magharibi, hasa Marekani, zimechochea moto wa vita kwa kutuma silaha za mabilioni ya dola kwa Ukraine.

Hali hii imezidisha mzozo.

Wiki iliyopita, China ilitoa wito wa kusitisha mapigano huku ikitoa mpango wa amani wa kumaliza vita nchini Ukraine.

Pendekezo hilo, ambalo linajumuisha vipengele 12, linazingatia kanuni ya kuheshimiwa mamlaka ya nchi zote mbili na linataka kuanzishwa tena mazungumzo ya amani na kuhimiza ujenzi mpya wa muda mrefu baada ya vita.

Beijing pia imetaka kuondolewa vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Russia na pia imekosoa sera za NATO za kuendelea kujipanua ikisema Marekani na NATO zinachochea moto wa vita na kwamba zina hatia kama waanzilishi wa mgogoro huo.

China pia imeweka wazi upinzani wake, sio tu kwa matumizi ya silaha za nyuklia, bali pia kwa tishio la kuzipeleka katika maeneo ya vita, ikisisitiza kwamba silaha za nyuklia hazipaswi kutumika.

Mbali na hayo, China imetoa wito kwa juhudi za kuweka korido za kibinadamu kwa ajili ya kuwahamisha raia kutoka maeneo yenye migogoro, kuwalinda raia na wafungwa wa vita, na kuwezesha usafirishaji wa nafaka nje ya nchi.China imejiweka kama upande usioegemea upande wowote katika mzozo huo na kuchukua nafasi ya mpatanishi.

Wakati huo huo, Russia imesema imetilia maanani sana mpango huo wa China lakini imesema masharti ya kusuluhisha mzozo huo kwa njia ya amani hayajabainika kikamilifu.

Moscow imesema kuwa suluhu yoyote ya mzozo huo inapaswa kutambua udhibiti wa Russia katika maeneo manne ya Ukraine yaliyojitenga mwaka jana. Pia inaitaka Ukraine kukataa ombi la Wamagharibi la kujiunga na NATO.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema nchi yake itachunguza mpango huo wa China lakini amesema kuwa haitakubaliana na mpango wowote wa amani kabla ya kurejea maeneo yote yaliyojitenga na kujiunga na Russia.

Kuchapishwa kwa pendekezo hilo kunafuatia shutuma kutoka kwa nchi za Magharibi kwamba China inafikiria kuipa Russiai silaha, madai ambayo Beijing imeyakanusha na kuyataja kuwa habari za uwongo.



342/