Kitengo cha habari cha Ikulu ya Kremlin kilitangaza jana Jumatano kwamba Jumanne jioni, Ukraine ilijaribu kumuua Rais Vladimir Putin wa Rusia kwa kufanya shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye Ikulu ya Kremlin.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kremlin, ndege mbili zisizo na rubani zilizokuwa zinaelekea Ikulu ya Kremlin, zilitunguliwa na mifumo ya vita ya kielektroniki ya huduma za usalama za Russia, na shambulio hili halikusababisha maafa yoyote ya roho na mali.
Kitengo hicho cha habari ya ofisi ya Rais wa Russia kimetangaza pia, kwamba Putin hakuwepo katika Ikulu ya Kremlin wakati wa shambulio hilo.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Dmiry Medvedev, rais wa zamani wa Russia akiandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Telegram Jumatano jioni kwamba: Shambulio hilo ni la kigaidi na halikubaikishia Moscow chaguo jingine isipokuwa kumuondoa katika uso wa dunia Zelensky na wenzake.
Amesisitiza kuwa: "Hakuna haja ya Zelensky kutia saini hati ya kujisalimisha bila ya masharti kwa sababu Hitler pia hakutia saini hati kama hiyo, na kwamba muda wote ziko njia mbadala za kuwaondoa duniani watu kama Hitler."
Kwa upande wake, Rais wa Ukraine jana Jumatano alikanusha kuhusika Kiev na shambulio la ndege zisizo na rubani kwenye Ikulu ya Kremlin huko Moscow, mji mkuu wa Russia.
342/