Jenerali Amos Gileadi, afisa mkuu mstaafu wa Jeshi la Israel ambaye aliwahi kuhudumu kama mkuu wa Kitengo cha Utafiti wa Kijasusi wa Kijeshi, alisema katika mahojiano ya redio kwamba "Wairani sasa wanahisi kuwa Israeli imedhoofika."
Raz Zimmt, mtaalamu mwandamizi wa Israel kuhusu Iran, pia alibainisha kuwa safari ya Raisi nchini Syria ni hatua inayoonyesha ushawishi mkubwa wa Iran. Aidha amesema kwa makubaliano muhimu ya kiuchumi kati ya pande hizo mbili, ni "mafanikio" kwa kambi ya 'muqawama'.
Mwandishi wa masuala yake ya kijeshi wa gazeti la kila siku la Israel Yediot Aharonot pia alielezea ziara hiyo kama "fursa iliyopotea" kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Maoni hayo yanakuja kufuatia mahojiano ya Rais Raisi na mtandao wa televisheni wa al-Mayadeen wa Lebanon siku ya Jumanne, Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Iran alisema: Hali ya mambo hivi sasa imebadilika na kwamba utawala wa Kizayuni hauwezi kujidhaminia usalama ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.
Rais wa Iran aliashiria matatizo ya ndani yanayouzonga utawala wa Kizayuni na kuongeza kuwa: Mikataba kama ule wa Sharam- Sheikh, wa Oslo na Camp David haiwezi kuudhaminia utawala huo usalama. Alisema,leo hii uamuzi uko mikononi mwa mujahidina wa Kipalestina na si katika meza ya mazungumzo ya kisiasa.
Akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa kisiasa na kiuchumi, rais wa Iran aliwasili Syria kwa mwaliko rasmi na mwenzake wa Syria siku ya Jumatano.
Alilakiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Damascus na Waziri wa Uchumi na Biashara ya Nje wa Syria Mohammad Samer al-Khalil. Baadaye alikaribishwa ramsi na mwenyeji wake, Rais Bashar al Assad katika Ikulu ya Damascus.
342/