6 Agosti 2023 - 20:06
Miaka mitatu baada ya mlipuko wa Beirut bado kesi ya kadhia hii haijatatuliwa

Ikiwa imetimia miaka mitatu tokea kujiri mlipuko wa kutisha huko Beirut mchakato wa mahakama katika kesi ya mlipuko huo bado haujakamilika na Lebanon bado inatawaliwa na serikali ya mpito.

Ilikuwa Agosti 4, 2020, wakati mlipuko mkubwa ulitokea huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon. Mlipuko huo ulitokea kutokana na kuzuka moto katika ghala moja huko katika bandari ya Beirut ambako kemikali zilikuwa zimehifadhiwa tangu 2013. Kutokana na mlipuko huo, zaidi ya watu 220 waliuawa na zaidi ya wengine 6,500 kujeruhiwa. Aidha mlipuko huo ulisababisha uharibifu mkubwa.

Miaka mitatu baada ya mlipuko huo mkubwa, Lebanon bado haina utulivu. Familia za waathiriwa bado zinasubiri haki kwa wahanga wa mlipuko huo. Kuhusiana na hilo, katika mkesha wa kuadhimisha mwaka wa tatu wa mlipuko wa Beirut, mamia ya watu wa Lebanon, pamoja na familia za wahanga wa tukio hilo wakiwa pamoja na wabunge wa sasa na wa zamani wa Bunge la Lebanon, wameshiriki katika maandamano wakitaka kuharakishwa mchakato wa kimahakama wa kesi na kuhukumiwa waliosababisha mlipuko huo.

Inaonekana kwamba kama vile chanzo cha mlipuko huo kilitazamwa kisiasa katika siku za mwanzo, mchakato wa mahakama wa kesi pia unaathiriwa na mielekeo ya kisiasa.

Mrengo wa kisiasa unaopinga kambi ya muqawama inayoongozwa na Harakati ya Hizbullah, mrengo ambao pia unaungwa mkono kutoka nje ya Lebanon, ulijaribu kuituhumi kambi ya muqawama kuwa ndiyo iliyohusika na mlipuko huo katika bandari ya Beirut, na njama hizo bado zinaendelea hadi hii leo.Seyyed Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon katika maadhimisho ya mwaka wa tatu wa maafa hayo akizungumzia kushindwa kwa njama ya Marekani ya kuituhumu Hizbullah amesema kuwa wale waliolitia siasa suala hili na kulihusisha na mchakato wa matukio ya kieneo pia walizuia kubainika ukweli kuhusu tukio hilo. Kuhusiana na nukta hii, Sheikh Ali Damush, naibu mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon amesema: "Tatizo kubwa zaidi lililokabili kadhia ya mlipuko wa bandari ya Beirut ni ufyonzaji wa kisiasa wa damu za wahanga, upotoshaji na kuficha ukweli kwa maslahi ya kisiasa." Ibrahim Hoteit msemaji wa kamati ya familia za wahanga wa mlipuko wa Beirut, alitangaza katika kumbukumbu ya miaka mitatu ya mlipuko huo mkubwa, kwamba baada ya miaka 3, kila mtu anasubiri kuona nini kitatokea na hakuna haki imetendeka kufikia sasa. Sababu kuu ni uwekezaji wa kisiasa wa baadhi ya vyama katika kesi ya mlipuko wa Beirut, na kuingilia vyama vya siasa katika kesi hii kumeibua tofauti kati ya familia za wahasiriwa. Jambo lingine muhimu ni kwamba miaka mitatu baada ya mlipuko wa bandari ya Beirut, Lebanon bado inatawaliwa na serikali ya mpito. Serikali ya Hassan Diab ilikuwa ya muda mfupi, Saad Hariri alishindwa kuunda baraza la mawaziri na Najib Mikati aliteuliwa kuunda baraza la mawaziri kuanzia Agosti 2022 baada ya muda mfupi, lakini baada ya mwaka mmoja kupita, bado hajafanikiwa kufanya hivyo. Hali ya sasa ya Lebanon ni kwa manufaa ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani, ambazo zinataka kuwepo serikali dhaifu na ya muda katika nchi hii. Uingiliaji wa kigeni katika mchakato wa kesi ya mlipuko wa Beirut, pia unachukuliwa kuwa sababu muhimu ya kushindwa kuundwa baraza jipya la mawaziri la Lebanon.

342/